Mwandishi Habari na Mtangazaji wa ITV Apigwa Risasi

Ufoo Saro (kulia) akipeana mkono na Rais Jakaya Kikwete.

Ufoo Saro (kulia) akipeana mkono na Rais Jakaya Kikwete.

*Mama Mzazi wa Ufoo Saro Auwawa kwa risasi

RAIS Kikwete (kushoto) akipena mkono na Ufoo Saro, alipokutana na Waandishi na Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari Ikulu jijini Dar es Salaam, Desemba 2012. (picha: Bayana blog).

IMERIPOTIWA kuwa mtu mmoja anayedaiwa kuwa alikuwa mume mtarajiwa (mchumba) wa Ufoo Saro aliyefahamika kwa jina la Ateri Mushi, amempiga risasi mwandishi wa habari na ripota wa ITV, Ufoo Saro na Anastazia Saro (mama mazazi wa Ufoo Saro) na kisha  kujipiga risasi mwenyewe.

Akizungumza na Ruben Mchome, Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Wambura amesema tukio hilo limetokea majira ya alfajiri ya leo. Mwanaume aliyefanya mauaji hayo alikuwa anafanya kazi katika Shirika la Umoja wa Mataifa (UN) nchini Sudan. Haijafahamika mapema bado kuwa alikuwa akifanya kazi gani wala katika kitengo gani.

Kamanda Wambura amasema inasemekana kulikua kuna ugomvi kati ya wawili hao ambapo walishindwa kuelewana na ndipo walipoamua kwenda kwa mama mzazi wa Ufoo Saro (mama mkwe). Alipofika huko inadaiwa kuwa mwanaume huyo alimshutumu mama mkwe wake kwamba anamtetea mwanaye (Ufoo Saro). Ndipo mwanaume huyo alipotoa bastola na kumpiga mama wa Ufoo Saro risasi kifuani na kumuua papo hapo na kisha akampiga Ufoo Saro risasi ya mbili, moja ya tumboni na nyingine mguuni. Inasadikiwa kuwa kwa kudhani kwamba amewaua wote, ndipo naye alipojifyatulia risasi kidevuni na kufariki dunia hapo hapo. (via MchomeBlog.com/Radio One)

Nukuu nyingine kutoka kwenye mitandao jamii zinasema, akizungumza kwa njia ya simu, Steven Chuwa wa ITV amesema tukio hilo limetokea kwenye nyumba alikokuwa akiishi mama wa Ufoo Saro, Kimbamba nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.

Imeelezwa kuwa  Ufoo alikimbizwa katika hospitali teule ya Tumbi (Kibaha) katika jitihada za kuuokoa uhai wake na baadaye alihamishiwa kwenye hospitali ya Taifa ya Muhimbili katika kitengo cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU).

Taarifa nyingine zinasema Mushi aliwasili nchini jana na  kufikia nyumbani kwa Ufoo alfajiri ya leo na kisha wawili hao ndipo walipoondoka kuelekea nyumbani kwa mama mzazi wa Ufoo ili kutafuta suluhisho la kutoelewana kwao.

CHANZO http://www.wavuti.com