Mwandishi Wetu, Shinyanga
MWANDISHI wa habari wa Kituo cha Televisheni ya ‘Channel Ten’ Mkoani Shinyanga, Charles Hilila amefariki dunia usiku wa kuamkia jana akiwa amelazwa hospitalini. Kwa mujibu wa taarifa ambazo mtandao huu umezipata baada ya kufanya mahojiano na mmoja wa waandishi wa habari waandamizi Mjini Shinyanga, Hilila alikuwa amelazwa katika Hospitali ya Mkoa huo na alikuwa akisumbuliwa na homa.
Alisema takribani amelazwa kwa wiki mbili katika hospitali hiyo ya mkoa kabla ya mauti kumkumba jana. Mwanahabari huyo alisema shughuli za mazishi ya Hilila zinaratibiwa na Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Shinyanga kwa kushirikiana na wanafamilia na anatarajiwa kuzikwa eneo la Tinde nje kidogo ya Mji wa Shinyanga.
Mwanahabari Hilila atakumbukwa kwa mengi hasa katika upiganiaji haki za wananchi mjini na vijijini kupitia taaluma yake kama mwanahabari na mchango mkubwa kupigania maslahi ya wanahabari mkoani humo. Marehemu Charles Hilila ameacha mke na watoto watatu. Mtandao huu unatoa pole kwa familia, Klabu ya Wanahabari mkoa pamoja na tasnia nzima ya wanahabari kwa kuondokewa na ‘Jembe Hilila’.
“Bwana ametwaa na jina lake lihimidiwe, Upumzike kwa amani Charles Hilila”