Na Mwandishi Wetu
MMILIKI wa banda moja la maonesho ya wanyama wakali akiwemo Simba, Aleksandr Pylyshenko ameamua kujifungia banda moja na Simba kaadhaa anaowamiliki ili kuvutia wateja (watalii) wa wanyama hao kwenye biashara yake.
Tukio hilo limetokea mwishoni mwa wiki mjini Vasilyevka Kusini Mashariki mwa nchi ya Ukraine, ambapo mmiliki huyo wa mbuga za wanyama hao wakali aliamua kuingia kwenye banda la simba na kuishi nao kwa wiki tano mfululizo akiwa amejifungia na wanyama hao wakali.
Taarifa zinasema Pylyshenko alijifungia katika banda moja na simba wawili dume na jike ambao wote ni asili ya Afrika wakiwa na majina ya Katya (simba jike) na Samson ( simba dume), kwa lengo la kupata fedha za kuweza kuwahudumia na kuwaboreshea maisha wanyama wake.
Mmiliki huyo wa wanyama hao ambaye pia ni mwanasanaa, mbali na kuishi na wanyama hao banda moja alikuwa akicheza nao kwa kuwabusu na kulala nao bila woga wowote, kitendo ambacho kiliwaogofya wengi.