Mwanasheria Mkuu Avitaka Vyama vya Siasa Kuacha ‘Ubabe’

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju (kushoto) akibadilishana mawazo na baadhi ya wahariri.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju (kushoto) akibadilishana mawazo na baadhi ya wahariri.

Na Hassan Silayo, MAELEZO

VYAMA vya siasa nchini vimetakiwa kutumia vyema haki zao za msingi zilizoanishwa katika katiba badala ya kutumia nguvu, ubabe hali inayotishia amani ana utulivu iliyopo nchini.

Kauli hiyo imetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju wakati wa mkutano wake na Wahariri wa vyombo vya habari akizungumzia kuhusu wajibu wa utii wa sheria na kudumisha amani nchini.

Mhe. Masaju alisema kumekuwa na baadhi ya wanasiasa wanaotoa vitisho vya kuitisha mikutano kinyume na taratibu za kisheria kwa kisingizio cha haki za kikatiba jambo ambalo sio kweli.

“Napenda kuvishauri vyama vya siasa nchini kuacha kutumia kauli za kibabe na vitisho kwa kisingizio cha kutumia haki zao za kikatiba, hali hiyo itapelekea vyombo vya dola kuchukua hatua kwani ni viashiria vya uvunjifu wa amani”.

Masaju aliwataka Wanasiasa kuwa wakweli na kuacha kuwapotosha wananchi kuwa wananyimwa haki ya kufanya mikutano kwani wapo baadhi yao wanaofanya mikutano katika majimbo yao baada ya Jeshi la Polisi kujidhirisha kwamba kutakuwa na hali ya amani na utulivu”. Alisema Mhe. Masaju.

Aidha Masaju alipongeza juhudi zinazofanywa na viongozi mbalimbali wa dini nchini kwa jitihada wanazofanya za kushauri katika kufika muafaka wa hali ya kisiasa nchini na kuwashauri kuhubiri amani na utulivu kwa waumini wao.

Akitoa ufafanuzi wa tamko la baadhi ya vyama vya upinzani kutaka serikali kuvifuta vyama hivyo Mhe. Masaju alisema kuwa suala hilo ni kinyume na katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa sababu katiba hiyo inaruhusu mfumo wa vyama vingi.