Mwananchi alipukiwa na bomu Lindi

Na Mwandishi Wetu
Lindi

MKAZI mmoja wa kijiji cha Kitumbikwera mkoani Lindi, Omari Said (29) amelazwa katika

Hospitali ya Mkoa ya Sokoine akiuguza majeraha aliyoyapata baada ya kulipukiwa na kitu

kinachosadikiwa kuwa ni bomu.

Tukio hilo limetokea hivi karibuni mjini hapa na majeruhi amelazwa wodi namba sita ambapo

ameumia vibaya sehemu ya mgongoni, ubavuni, matakoni pamoja na kukatika kiganja cha mkoni wa

kulia.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Sifuel

Shirima alisema mtu huyo ambaye ni mvuvi amejeruhiwa na mlipuko huo majira ya saa tano

asubuhi kwenye Bahari ya Hindi alipokuwa akivua samaki.

Alisema, mvuvi huyo ambaye alijipeleka mwenyewe kituo cha Polisi kwa ajili ya kupatiwa hati

ya matibabu (PF3) alieleza kuwa, amelipukiwa na kitu alichodai alikiokota Pwani wakati

akielekea baharini kuvua samaki.

“Maelezo yake anadai wakati akielekea baharini kuvua kuna kitu alikiokota na alipochukuwa

kibiriti ili awashe sigara avute kile kitu kilimlipukia na kumjeruhi,” alisema Shirima

akinukuu maelezo ya mjeruhiwa huyo.

Kamanda huyo wa polisi alisema, pamoja na madai ya mvuvi huyo bado kwa upande wao

wanaendelea kufanya uchunguzi wa madai ya mvuvi huyo, kama kweli amelipukiwa na kitu

alichodai amekiokota au ni uvuvi haramu wa samaki uliotokana na matumizi ya baruti.

Aidha, huyo ni mvuvi wa pili kulipukiwa na baruti inayotokana na uvuvi haramu kwani mwaka

jana pia mkazi wa kijiji hicho amepoteza baadhi ya viungo vyake baada ya kulipukiwa na

baruti kutokana na uvuvi huo.

mwisho.

Wanne wapandishwa kizimbani kwa dawa za kulevya

Na Mwandishi Wetu

RAIA wanne wa mataifa tofauti, jana wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi

Kisutu, kwa kosa la kula njama na kuingiza dawa za kulevya nchini zenye thamani ya sh

bilioni 2.8.

washtakiwa hao ambao ni Dennis Okechukwa, Paul Obi ambao ni raia wa Nigeria, mwingine ni

raia wa Afrika Kusini, Stani Hycenth pamoja na raia wa nchini Pakistan ambaye alitajwa kwa

jina la Shoaib Ayaz, wote walisomewa mashtka mawili mahakamani hapo.

Wakili wa upande wa mashitaka, Prosper Mangamila akisaidina na Biswalo Mganga, walisoma

mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mustapher Syani, ambapo ilidaiwa katika shtaka la kwanza

washtakiwa hao wanatuhumiwa kwa kosa la kula njama.

Mwangamila alidai katika siku tofauti kati ya Septemba 26, mwaka jana na Machi 4, mwaka huu

katika maeneo tofauti katika nchi za Tanzania, Nigeria, Afrika Kusini na katika maeneo

tofauti nchini Pakistan washtakiwa hao walikula njama ya kutaka kusafirisha dawa za kulevya

kwa nia ya kuleta nchini.

Alidai katika shtaka la pili ambalo watuhumiwa hao wanatuhumiwa kusafirisha dawa za kulevya,

ilidiwa Machi 4 mwaka huu, huko Kunduchi Mtongani washtakiwa kwa pamoja waliingiza nchini

dawa za kulevya aina ya Heroine gramu 81,000 zenye thamani ya sh 2,835,000,000.

Wakili anayewatetea washtakiwa hao Braison Shayo, aliiomba mahakama kutoa kibali cha

washtakiwa hao kurudishiwa simu zao ili wawasiliane na ndugu zao kwakuwa washtakiwa hao si

raia wa Tanzania.

Hoja hiyo ilipingwa na mawakili wa upande wa mashitaka, ambapo alidai wakili huyo ametumia

kifungu gani cha sheria na kwamba hakuna sheria inayoruhusu vitu vilivyokamatwa kwa ajili ya

uchunguzi kurudishwa kwa mshtakiwa.

Mganga alidai kimsingi mahakama hiyo haina mamlaka ya kutoa au kuruhusu mali hizo kurudishwa

kwa mshtakiwa kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na mamlaka ya kusikiliza shauri hilo.

Wakili huyo wa upande wa mashtaka aliendelea kudai kifungu 38 cha sheria ya makosa ya

mwenendo wa jinai (CPA), kinamruhusu Polisi kukusanya vifaa ambavyo wanaona vinafaa katika

uchunguzi na kwamba kurudishwa kwa mawasiliano kwa washtakiwa hao kutaharibu mwenendo wa

ushahidi kwakuwa kesi hiyo bado inafanyiwa uchunguzi zaidi.

Mahakama ilitoa uamuzi wake, ambapo ilisema haina mamlaka ya kutoa uamuzi wowote kwa hayo

maombi wanayotaka na kwamba wanaweza kuyapeleka Mahakama Kuu ambayo ndio yenye mamlaka ya

kusikiliza shauri hilo, kesi hiyo imehairishwa hadi Machi 21, mwaka huu.