Mwanahabari mkongwe nchini, Simon Mkina ambaye amewahi kuwa mhariri wa magazeti mbalimbali ndani na nje ya Tanzania amepata ajali ya gari.
Mkina amepata ajali hiyo jana usiku jijini Dar es Salaam akitokea katikati ya mji kuelekea nyumbani kwake Bunju, baada ya gari lake namba T 588 BPN aina ya Daihatsu kugonga nguzo ya umeme alipokuwa akijaribu kukwepa lori ambalo lilikuwa limeegeshwa katikati ya barabara baada ya kuharibika bila ishara yoyote.
Akizungumza kwa tabu na mwandishi wa habari hizi, Mkina alisema ajali hiyo ilitokea alipokuwa na mkewe akitokea mjini jana usiku na gafla alilikuta lori ambalo lilikuwa limeegeshwa barabarani, hivyo katika jitihada za kulikwepa aligonga nguzo na gari kuharibika vibaya mbele.
“Ulikuwa ni usiku na yaelekea lori hilo lilikuwa limeharibika na limeacha barabarani hakukuwa na ishara yoyote alafu ni giza mimi nililiona ghafla nikiwa karibu, nikijitahidi kukwepa niliingia kushoto kwangu na kugonga nguzo ya umeme…,” alisema Mkina.
Mkina ambaye baada ya ajali alipelekwa kwenye Hospitali ya Imtu iliyopo eneo la Mbezi Beach jijini Dar es Salaam ameruhusiwa leo na anaendelea na matibabu nyumbani kwake Karibu na Kituo cha Polisi Bunju.
Wakizungumza ndugu wa karibu wa Mkina ambao walimpeleka hospitali walisema kwa mujibu wa maelezo ya madaktari, yaelekea amepata maumivu kifuani ambapo alipigwa na usikani baada ya ajali hiyo. Hata hivyo hali ya mkewe ambaye alikuwa naye kwenye ajali hiyo inaendelea vizuri.
Mkina amewahi kuwa mhariri wa habari katika magazeti mbalimbali hapa nchini na nje ya nchi, yakiwemo magazeti ya Uhuru, Habari Leo, Kulikoni, Jambo Leo, Zanzibar Leo na pia kufanya kazi katika taasisi inayofadhili vyombo vya habari na wanahabari katika kutimiza majukumu yao (Tanzania Media Fund).
Mkina ambaye ni mwanahabari mkongwe kwa sasa amejiunga na timu ya dev.kisakuzi.com mwezi mmoja uliopita na anafanya kazi kama Mhariri Mtendaji na Kiongozi Mkuu wa website hiyo Tanzania.