Na Mwandishi Wetu, Mbeya
MWANDISHI wa habari mbobezi wa masuala ya Afya ya uzazi na dawa za kulevya nchini, Gordon Kalulunga, leo amechukua fomu ya kuwania Ubunge katika jimbo la Mbeya Vijiini mkoni Mbeya, kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Akizungumza na waandishi wa habari ambao walifika katika ofisi za CCM za wilaya hiyo zilizopo eneo la Sabasaba Jijini Mbeya, Kalulunga alisema amefikia hatua hiyo ikiwa kwanza ni kutimiza haki yake ya kikatiba na haki ya mwanachama wa CCM.
Mgombea huyo kijana, alisema umefika wakati wa kuiuisha CCM katika asili yake ya kuwa chama cha wakulima na wafanyakazi badala ya kuwa chama cha wafanyabiashara na watoa rushwa.
“Nawachukia kweli wagombea watoa rushwa ambao wapambe wao wakiulizwa wanadai ni moja ya njia za ushindi! Hii siyo CCM ninayoitaka ambayo wale ambao hawajapata baadae wanakichukia chama. Mbeya vijijini ina mahitaji ya kimaendeleo, na mimi kama kijana ndiye ninafaa kukivusha chama salama na kuiletea maendeleo wilaya yetu kwa kushirikiana na wananchi tena wa vyama vyote” alisema Kalulunga.
Mwandishi huyo ambaye pia ni Mjumbe wa mkutano mkuu wa taifa UVCCM na mjumbe wa Baraza na kamati ya utekelezaji UVCCM Mkoa wa Mbeya, anasema umefika wakati wa kuiona Mbeya vijijini ikiwa na vyuo, bei nzuri ya zao la pareto, wananchi kujiunga na bima ya Afya ya jamii sambamba na utolewaji wa huduma nzuri za afya, vyoo vya wanafunzi vizuri na mambo yafananayo na hayo bila kusahau viongozi kila mara kukutana na wananchi na vijiiini mapato na matumizi kuhakikisha yanasomwa kila baada ya miezi mitatu.
“Wengi wananiuliza kwanini nimeingia kwenye kinyang’anyilo cha nafasi ya Ubunge nikiwa kijana wa miaka 31 na sina fedha za kuhonga? Nawaambia kuwa maandiko yamesema mtu asiudharau ujana wako na zamani iliwahi kutabiriwa kuwa, nyakati hizi vijana tutakuwa na maono, wazee wataota ndoto” anasema Kalulunga.
Mpaka kufikia leo majira ya saa sita mchana, katika jimbo hilo wagombea 12 walikuwa tayari wamechukua fomu wakiongozwa na Mbunge anayetaka kutetea nafasi hiyo, Mch. Luckson Mwanjale.
Wengine ni mwenyekiti wa Halmashauri ya Mbeya, Anderson Kabenga, Japhet Mwanasenga ambaye ni mtumishi wa shirika la Nyumba la Taifa, Oran Njeza ambaye ni mstaafu wa masuala ya fedha nchini Nigeria, Kasim Chaka Chaka na wengine waliotajwa kwa jina la Mwalwego na Boniface.