Mwanahabari Edson Kamukara Afariki Dunia…!

Mwandishi wa Habari, Edson Kamukara

Mwandishi wa Habari, Edson Kamukara

Na Joachim Mushi
MWANDISHI wa habari Edson Kamukara aliyekuwa mfanyakazi wa Hali Halisi Publishers Limited (HHPL) amefariki dunia ghafla nyumbani kwake Mabibo jijini Dar es Salaam. Edson ambaye kwa sasa alikuwa Mhariri wa gazeti tando la MwanaHALISI ONLINE amefariki dunia majira ya saa kumi na mbili jioni huku taarifa za awali zikieleza kifo chake kimetokana na kulipukiwa na jiko la gesi.

Baadhi ya majirani wanasema kabla ya kifo cha mwanahabari huyo alianguka akiwa njiani kuelekea dukani na kumpa msaada hadi nyumbani kwake na akaomba apumzike kwani alikuwa amezinduka na anajielewa. Baada ya hapo walimuacha nyumbani kwake lakini baada ya muda walisikia vyombo vikivunjwa ndani kwake kana kwamba kulikuwa na mapambano au alikuwa akivunja vyombo hivyo mwenyewe.

Majirani wanasema baada ya purukushani hizo waliitwa watu na kuingia ndani ambapo walimkuta akiwa ameanguka chini huku akivuja damu sehemu ya kichwani na baadhi ya vyombo vya udongo kuvunjwa ikiwemo televisheni huku akiwa ajitambui na flana aliyokuwa ameivaa ilikuwa imeungua sehemu za juu. Jiko la gesi lilikuwa limeanguka chini na mwili wake kuonekana umeungua sehemu za usoni na mikononi pia damu kutapakaa baadhi ya sehemu ndani kwake.

Baadhi wanasema huenda malaria ilimpanda kichwani kisha kuanza kufanya fujo mwenyewe hivyo kujikuta akijijeruhi na jiko la gesi kumlipukia na kusababisha majeraha kabla ya uhai kumtoka. Hata hivyo Polisi wa kituo cha Magomeni walifika nyumbani kwa Edson kuchukua mwili huo na kufanya uchunguzi wa awali wakitafuta chazo cha kifo chake.

Thehabari.com ilifanikiwa kufika eneo la tukio na kukuta baadhi ya vyombo ikiwemo televisheni kuvunjwa na kutapakaa chumbani na jikoni huku jiko la gesi likiwa limeanguka na damu zikiwa zimetapakaa baadhi ya maeneo hasa jikoni kwake. Uchunguzi wa kifo chake bado unaendelea. Hata hivyo baadhi ya ndugu wa Edson wakiwa eneo la tukio walisema huenda kulikuwa na mapambano kabla ya marehemu kufariki dunia lakini bado haijajulikana yalikuwa ya nini.

Mwili wa Kamukara umehifadhiwa katika Hospitali ya Muhimbili ilhali jeshi la polisi likijaribu kutafuta chanzo cha kifo cha mwanahabari huyo, na msiba upo nyumbani kwa Dada yake Mkubwa Makongo Juu jijini Dar es Salaam kabla ya kufika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) Makongo.

Mkurugenzi Mtendaji wa HHPL, wachapishaji wa magazeti ya MwanaHALISI, MSETO, MwanaHALISI ONLINE na mtandao wa MwanaHALISI Forum, Saed Kubenea amethibitisha kifo cha mwandishi huyo na kusema: “Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kuondokewa na mwenzetu Kamukara ambaye tulimfahamu na kumpenda. Nilianza kufahamiana na Kamukara wakati akiwa gazeti la Tanzania Daima. Namfahamu kama mchapakazi, mwadilifu na mkweli. Alikuwa anashindana kwa hoja.

Kubenea anakiri kuwa Kamukara alimjulisha anasumbuliwa na malaria akiwa Bukoba safarini alipokwenda kumjulia hali mamayake mzazi ambaye alikuwa mgonjwa. Kubenea anasema alimsihi apumzike na kupata matibabu ya kutosha.
Katika maisha yake ya uandishi wa habari, Kamukara alifanya kazi katika magazeti mbalimbali yakiwemo Majira, Jambo Leo na Tanzania Daima kabla ya kujiunga na MwanaHALISI ONLINE, Februari mwaka huu.

Mtandao huu unatoa pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki wa Edson Kamukara katika kipindi hiki cha majonzi. Bwana ametoa na Bwana ametwaa jina lake lihimidiwe, Amina.