Mwanafunzi Miaka 13 Msingi Abebeshwa Mimba, Afaulu Sekondari…!

Mwanafunzi huyo akiwa na mwanaye akizungumza na mwanahabari Joachim Mushi, Kijijini Newala

Mwanafunzi huyo akiwa na mwanaye akizungumza na mwanahabari Joachim Mushi, Kijijini Newala

Na Joachim Mushi, Newala
MIMBA za umri mdogo ambazo zimekuwa zikiwakatisha wanafunzi masomo Wilaya ya Newala, mkoani Mtwara bado ni tatizo. Matukio ya mimba hizi kwa wanafunzi mbali ya kuwakatisha masomo yao zimekuwa zikitishia afya zao pia. Fatuma Rashid, 14(si jina lake halisi) ni mwanafunzi wa Shule ya Msingi Kipimi, Kata ya Makote Wilayani Newala ambaye alimaliza elimu ya darasa la saba Septemba 2013 huku akiwa mjamzito pasipo walimu kujua.
Baada ya matokeo kutoka Fatuma amejikuta amechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Makote Day iliyopo Kata ya Makote, lakini ameshindwa kuendelea na shule baada ya mimba kumkatisha masomo yake. Uchunguzi unaonesha Farida alipata ujauzito tangu mwezi Agosti 2013 na alianza kuhudhuria kliniki kwa siri huku akiendelea na masomo yake ya msingi hadi alipofanya mitihani yake ya mwisho shule ya msingi iliyofanyika Septemba 19 na 20, 2013.
Taarifa zinaonesha farida alisajiliwa katika daftari la wajawazito Zahanati ya Makote tangu mwezi wa Agosti 2013 ambapo alieleza kuwa ana umri wa miaka 13. Hata hivyo baada ya kurudi nyumbani alibadili umri wake kwenye kadi ya kliniki ya waja wazito na kuandika kwa wino mweusi kuwa alikuwa na miaka 15 badala ya 13 aliyotaja mwenyewe siku ya kwanza kliniki.
Hata hivyo akiwa anaenda katika mahudhurio ya kliniki akilea mimba yake alifanikiwa kubadili tena umri wake katika kitabu cha zahanati na kuandika umri wa miaka 15. Haikujulikana alimshawishi nini nesi hadi kumbadilishia umri na kumuongezea miaka miaka miwili.
Mwandishi wa makala haya alifanikiwa kupata kadi ya kliniki ya mama ambayo ilionesha wazi kuwa umri ulioandikwa awali ilikuwa ni miaka 13 kwa wino wa bluu lakini sasa umebadilishwa na kwenye tatu kuandikwa 5 kwa wino mweusi. Mtoto Farida amefanikiwa kujifungua mtoto wa kiume Aprili 24, 2014 katika Hospitali ya Wilaya ya Newala na kwa sasa analea mtoto akiwa nyumbani kwa shangazi yake Kijiji cha Kipimi.
Mazungumzo ya Fatuma na mwandishi wa makala haya yaliyofanyika mwezi Mai, 2014 kijijini Kipimi anaeleza kuwa ana umri wa miaka 17 na anasema alizaliwa 1995 jambo ambalo kiuhalisia haliendani. Kama kweli Farida alizaliwa mwaka anaoutaja yeye (1995) alipaswa kuwa na miaka 19 na si 17 kama anavyosema.
Kimsingi inaonesha wazi kuwa taarifa anazozitoa juu ya umri wake ni za uongo, na yaelekea anafanya hivyo kwa makusudi kuficha umri mdogo alionao yaani miaka 14 tena akiwa mwanafunzi kubeba mimba. Fatuma akifafanua zaidi katika mazungumzo yake anaweka wazi kuwa alianza uhusiano wa kingono na Ramadhani Zawadi (26) ambaye ndiye baba wa mtoto aliyekatisha masomo ya Farida, tangu mwaka 2012 akiwa darasa la sita katika Shule ya Msingi Kipimi.

Baadhi ya wanafunzi wa Shule za Msingi Kipili waliozungumza na mwandishi wa makala haya.

Baadhi ya wanafunzi wa Shule za Msingi Kipili waliozungumza na mwandishi wa makala haya.

Taarifa iliyopatikana kutoka katika shule ya msingi aliyomaliza Fatuma zinathibitisha kuwa mwanafunzi huyo ni miongoni mwa mabinti waliochaguliwa kuendelea na masomo ya sekondari katika Shule ya Sekondari Makote Day, licha ya yeye kushindwa kuendelea na masomo kutokana na hali aliyonayo kwa sasa.
Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari Makote Day, Said Ntinika akizungumza na mwandishi wa makala haya alithibitisha kuwa Farida ni miongoni mwa wanafunzi waliochaguliwa katika shule hiyo kuendelea na masomo ya sekondari, lakini anasema hadi kufikia mwezi Mei mwishoni, 2014 alikuwa hajaripoti shuleni na shule haina taarifa zozote juu ya mwanafunzi huyo.
Matukio ya mimba utotoni hayajamuathiri Fatuma pekee wilayani Newala. Wapo wasichana wengi kama yeye ambao wanakatishwa masomo wakiwa shule za msingi au sekondari kutokana na matukio ya mimba katika umri mdogo.
Faudhia Hashim, 14 (si jina lake halisi) ni mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Makote Day, lakini mwanafunzi huyu ameshindwa kuendelea na masomo yake baada ya kupata ujauzito akiwa katika harakati za usajili kuingia shuleni.
Maimuna Said (30) ni Mkazi wa Kata ya Makote Wilaya ya Newala na miongoni mwa wazazi ambaye mtoto wake naye aliwahi pata mimba shule ya msingi. Mama huyu akizungumza, anasema alibaini mwanaye ni mjamzito akiwa katika mchakato wa kumsajili kuingia kidato cha kwanza Sekondari ya Makote Day baada ya kufaulu akitokea Shule ya Msingi Kipimi.
Anasema alikuwa katika hatua za mwisho kumsajili kujiunga na sekondari ndipo alibaini kuwa ni mjamzito baada ya majirani kumshauri kuwa akampime.
“…Walianza kumshitukia majirani zangu wakaniambia kabla ya kumpeleka huko sekondari alipochanguliwa nikampime mimba maana wao wanaona huenda akawa mjamzito kulingana na mabadiliko ambayo anayaonesha, nilimchukua na kumpeleka zahanati na baada ya kumpima waliniambia ni mjamzito…tangu nimeambiwa nimeshindwa nifanye nini lakini tayari nimemjulisha mjomba wake,” anasema Bi. Maimuna.
Katika mazungumzo na Faudhia anajaribu kuficha umri wake halisi kwa mwandishi, yeye anadai anaumri wa miaka 15 kauli ambayo inapingana na mmoja wa ndugu wa familia hiyo, ambaye anasema binti huyo ana miaka 14. Sijui ni kwanini binti huyu anajiongezea miaka. Huenda hii ni tabia ya mabinti wengi wa eneo hili wanaopata mimba utotoni kwa kile kuhalalisha wao kubeba ujauzito. Faudhia si wa kwanza, kuficha miaka yake halisi maana hata Fatuma alidanganya umri mwanzo wa makala haya.
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Newala, Dk. Yudas Ndungile anasema tatizo la mimba za umri mdogo au mimba utotoni ni kubwa kwa wastani eneo hilo. Anasema idadi ya wateja (wagonjwa) wanaokuja kujifungua hospitalini hapo chini ni umri wa miaka 18 ni wengi.
“…Kimsingi tatizo la mimba katika umri mdogo lipo na ni kubwa kwa wastani, idadi ya wanaokuja kujifungua wakiwa na umri wa chini ya miaka 18 ni wengi, wapo wengi na kwa utaratibu ambao tumejiwekea kwamba mama yeyote aliyepata ujauzito chini ya miaka 20 anapazwa kujifungulia katika hospitali ya wilaya au kwenye kituo cha afya. Tunafanya hivi maana endapo mtu huyu atapata matatizo wakati wa kujifungua kutokana na umri wake atafanyiwa upasuaji wa dharura,” anase Dk. Ndungile.
Anasema wajawazito wengi chini ya umri unaostahili wanaokuja kujifungua hupata tatizo la kushindwa kujifungua kwa njia ya kawaida, pia wanashindwa kuwajibika katika kutunza mtoto kama mama hasa siku za mwanzo na wengine hata kusababisha mtoto mchanga kupata maambukizi na hata kufariki. Anaongeza kuwa hata wanaofanikiwa kujifungua kwa njia ya kawaida nao hupata tatizo la kuchanika na kutokwa na damu nyingi wakati wakijifungua jambo ambalo anasema ni hatari kiafya.
Anasema ili kukabiliana na mimba za umri mdogo idara yake imejiwekea utaratibu wa kutoa elimu ya afya ya uzazi na malezi kwa njia ya ushauri katika zahanati, vituo vya afya na hospitali zoezo ambalo linafanyika muda wote wa huduma katika vitengo husika.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Newala, Bi. Christina Kambuga akizungumza na mwandishi wa makala haya (hayupo pichani)

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Newala, Bi. Christina Kambuga akizungumza na mwandishi wa makala haya (hayupo pichani)

Anasema mimba za umri mdogo eneo hilo zinachangiwa na mambo mengi ikiwemo hali ya kiuchumi (duni) kwa familia husika, elimu duni kwa jamii ambapo idadi kubwa ya wanaopata mimba za umri mdogo hawajafika sekondari na pia wazazi wanashindwa kutimiza wajibu wao kwa familia. Anabainisha idara yake pia inaendelea kutoa elimu kupitia majukwaa mbalimbali vikiwemo vikao vya wadau anuai wa elimu.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Newala, Bi. Christina Kambuga katika mazungumzo na mwandishi wa makala haya ofisini kwake, anakiri ukubwa wa tatizo la mimba utotoni hasa kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari katika eneo hilo.
“…Tatizo la mimba za utotoni hili limekuwa ni tatizo kubwa hasa kwa shule zetu za msingi na sekondari lakini hata na kwa jamii kwa ujumla, watoto waliowengi huku wanazaa chini ya umri unaostahili mpaka imefikia mahali kuna watoto wanazaa chini ya miaka 12, hili ni tatizo kubwa ambalo lipo hapa (Newala),” anasema.
Bi. Kambuga anasema tatizo kubwa linalochangia hali hiyo ni mmomonyoko wa maadili ambalo ni tatizo kubwa, likifuatiwa na suala la uendelezaji mila na desturi za watoto kushiriki katika jando wakiwa na umri mdogo. Kuanza kwa unyago na jandoni huko nyuma ilikuwa ni ujenzi wa maadili, na watoto walikuwa wanapelekwa huko wakiwa na umri mkubwa jambo ambalo kwa sasa linafanyika kinyume, hivyo watoto kupelekwa wakiwa na umri mdogo. Sasa unakuta uwezo wa kushika wanayofundishwa na kuyatafakari na hata kuyatumia wakati mwingine inakuwa ni tatizo. Yaani badala ya kuyatumia yanavyotakiwa yawe na kwa wakati wake watoto wamekuwa wakiyajaribu muda mfupo baada ya kutoka jandoni na unyagoni.
Anasema tatizo jingine ni jamii yenyewe kulea maovu ya mimba za utotoni. Wapo wazazi ambao hawatoi ushirikiano sheria zichukue mkondo wake pale inapotokea wanafunzi hawa wanabebeshwa mimba, na wazazi wengine wamekuwa hata wakiwashauri waliowapa mimba wanafunzi kutoroka mara baada ya kuona vyombo husika vinafuatilia.
Anasema wakati mwingine hata vyombo vya dola vinapojitahidi kufanya kazi yake na kufikisha kesi hizo mahakamani watoa ushahidi ambao ni watoto na wazazi wao wamekuwa wakigoma kuja mahakamani na kukwamisha ushaidi hivyo kushindwa kufanikiwa.
“…Binafsi naamini kama wangepatikana watu wa kutolewa mfano kila wanapofanya makosa haya ya kuwabebesha mimba wanafunzi watu wangeogopa kufanya vitendo hivi,” anasema mtendaji huyu mkuu wa wilaya ya Newala.
Anasema pamoja na hali hiyo sababu nyingine inayochangia kukithiri kwa mimba za utotoni ni pamoja na kufunjika kwa ndoa holela eneo hilo. Anasema ndoa zimekuwa zikifunjika hasa msimu wa mavuno ya korosho na watoto kubaki ama kwa bibi au kwa mama ambaye mara baada ya ndoa yake kuvunjika anaweza kuolewa tena na kuwaacha watoto wa awali bila uangalizi wa kutosha.
“…Unakuta watoto wanabaki kwa bibi ambapo wanakosa mahitaji ya msingi kutokana na uwezo mdogo wa bibi, mtoto analazimika kutafuta mwenyewe jambo ambalo linachangia kujikuta anapata mimba za umri mdogo kiurahisi kutokana na mazingira anayoishi huku akiwa hana uangalizi wa kutosha,” anabainisha Kaimu Mkurugenzi,” Bi. Kambuga.
Anasema ili kukabiliana na hali hiyo Serikali wilayani Newala imekuwa ikipambana kwa kutoa elimu kwa jamii kupitia viongozi wa ngazi mbalimbali pamoja na idara anuai eneo hilo.
“…Suala la elimu kwetu imekuwa ni ajenda ya kudumu katika gazi zote, kuanzia ngazi ya halmashauri za vijiji, kamati za maendeleo za kata na katika ngazi nyingine ni lazima tuwe na ajenda ya kuzungumzia suala hili. Wakati huo huo pia bado tunayo mabaraza ya kata ambayo tatizo kama hilo linapo tokea wajumbe hulishughulikia…na anapobainika mtia mimba huanza kufikishwa kwenye mabaraza haya,” anasema.
Hata hivyo takwimu kutoka Dawati la Jinsia na Watoto la Wilaya la Jeshi la Polisi linaonesha kuwa kuanzia Januari hadi Machi 2014 kuna jumla ya kesi nne (4) za wanafunzi kutiwa mimba na kukatishwa masomo na makosa mawili (2) ya watu walioshtakiwa kwa kuwaweka kinyumba wanafunzi. Ikiwa ni tafsiri ya kumzorotesha mwanafunzi masomo.
*Imeandaliwa na www.thehabari.com kwa kushirikiana na TAMWA