Mwana Mfalme wa Japan Atembelea Ikulu Dar

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akipokea hati ya utambulisho toka kwa Balozi wa Sri Lanka nchini Tanzania mwenye makazi yake jijini Nairobi, Kenya,  Dkt Velupilai Kananathan kwenye sherehe fupi zilizofanyika Ikulu jijini Dar es salaam July 3, 2014. PICHA NA IKULU.

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akipokea hati ya utambulisho toka kwa Balozi wa Sri Lanka nchini Tanzania mwenye makazi yake jijini Nairobi, Kenya, Dkt Velupilai Kananathan kwenye sherehe fupi zilizofanyika Ikulu jijini Dar es salaam July 3, 2014. PICHA NA IKULU.


RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, Julai 3, 2014, amemkaribisha Ikulu, Dar Es Salaam, Mwana wa Mfalme wa Japan, Prince Akishino pamoja na mkewe Princess Akishono. Mwana Mfamle huyo ambaye anatembelea Tanzania, amewasili Ikulu kiasi cha saa nne asubuhi na kufanya mazungumzo ya zaidi ya nusu saa na Mheshimiwa Rais Kikwete.

Katika mazungumzo yao, Rais Kikwete amesema kuwa Japan ni mshirika mkubwa na muhimu sana wa maendeleo ya Tanzania. “Tunathamini sana mchango wenu katika maendeleo ya Tanzania na tunaendelea kuwashukuru sana. Ukizunguka nchini mwetu utaona kwa macho yako miradi mingi na mikubwa ambayo imejengwa ama inajengwa kwa msaada wa Japan.”

Rais kikwete ameongeza: “Pamoja na ushirikiano huu. Bado tunaamini kuwa Japan inaweza kusaidia zaidi Tanzania hasa kwa kushawishi makampuni yake kuwekeza katika sekta binafsi. Ukipita mitaa ya Dar es Salaam, magari tisa kati ya 10 ni ya Kijapan. Ukiingia katika maduka ya vyombo vya elektroniki – televisheni, kompyuta, camera, karibu kila kitu kinatoka Japan. Hali hii inathibitisha kuwa bidhaa vya Japan zina soko kubwa na zinaweza kuzalishwa hata hapa nchini na makampuni binafsi.”
Rais Kikwete pia ameitaka Japan kuangalia jinsi gani inavyoweza kusaidia ongezeko la watalii kutoka Japan kuja kutembelea Tanzania kwa kuanzisha safari za ndege za moja kwa moja kutoka huko hadi Tanzania na nchi nyingine za Afrika.
“Wataalii wengi kutoka Japan wanashindwa kuja Afrika kwa sababu hakuna shirika hata moja la ndege la Japan ambalo lina safari za kuja Afrika, hata Afrika Kusini hakuna. Hii ndiyo maana hatuoni watalii wengine kutoka nchi za kusini mashariki mwa Bara la Asia kutembelea vivutio vyetu vya utalii,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Kama kuna jambo halionekani sasa katika uhusiano wa Tanzania na Japan ni uwekezaji katika sekta binafsi. Hili ndilo jambo tunaloliomba.”

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akimtambulisha kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mhe Bernand Membe Balozi wa  Poland nchini Tanzania mwenye makazi yake jijini Nairobi, Kenya, Marek Zial Kowski  kwenye sherehe fupi zilizofanyika Ikulu jijini Dar es salaam July 3, 2014

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akimtambulisha kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mhe Bernand Membe Balozi wa Poland nchini Tanzania mwenye makazi yake jijini Nairobi, Kenya, Marek Zial Kowski kwenye sherehe fupi zilizofanyika Ikulu jijini Dar es salaam July 3, 2014

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akipokea hati ya utambulisho toka kwa balozi wa Romania nchini Tanzania mwenye makazi yake jijini Nairobi, Kenya, Mhe Julia Pataki kwenye sherehe fupi zilizofanyika Ikulu jijini Dar es salaam July 3, 2014.

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akipokea hati ya utambulisho toka kwa balozi wa Romania nchini Tanzania mwenye makazi yake jijini Nairobi, Kenya, Mhe Julia Pataki kwenye sherehe fupi zilizofanyika Ikulu jijini Dar es salaam July 3, 2014.


Wakati huo huo Rais Kikwete, amepokea hati za utambulisho za mabalozi watatu ambao wataziwakilisha nchi zao katika Tanzania. Katika hafla fupi zilizofanyika Ikulu, Dar es Salaam, Rais Kikwete amepokea hati za utambulisho za Waheshimiwa Mabalozi Velupilai Kanathan wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kisoshalisti ya Sri Lanka, Marek Zial Kowski wa Poland na Julia Pataki wa Romania na kupata nafasi ya kuzungumza na mabalozi hao.

Pamoja na kumkaribisha Balozi Kanathan wa Sri Lanka nchini, Rais Kikwete ameishukuru nchi hiyo kwa ushirikiano wake na Tanzania katika kupambana na ugonjwa wa minazi ambao unaharibu zao hili kwa kukausha miti inayozalisha nazi.
“Kwa baadhi yetu ambao tunatoka maeneo yenye kulima nazi, zao hili ndilo maisha yetu na ndilo uchumi wetu. Sasa tunapoteza minazi yote kwa ugonjwa. Tunaishukuru sana Sri Lanka na Serikali yake kwa ushirikiano wake katika kukabiliana na ugonjwa huo,” amesema Rais Kikwete.

Balozi huyo mwenye makazi yake nchini Uganda amemwambia Rais Kikwete kuwa watalaam wengine wa zao la nazi watawasili nchini mwezi ujao kuendelea na kazi hiyo ya kupambana na ugonjwa wa zao la nazi. Rais Kikwete pia ameipongeza Sri Lanka kwa kuandaa vizuri na kwa ufanisi mkubwa Mkutano wa Wakuu wa Serikali za Jumuia ya Madola (CHOGM) uliofanyika mjini Colombo, nchini humu Novemba mwaka jana.

Katika mazungumzo yake na Mheshimiwa Balozi Kowsik wa Poland, Rais Kikwete amesema kuwa Tanzania imenufaika sana na ushirikiano wake na Poland kwa njia hasa ya mafunzo. “Wengi wa madaktari wetu na wahandisi wetu walipata elimu na mafunzo yao katika Poland. Tunawashukuru sana kwa msaada huo.”
Naye Balozi Kowsk amemwambia Rais Kikwete kuwa nchi hiyo inajiandaa kwa ajili ya ziara ya Waziri Mkuu wa nchi hiyo katika Tanzania iliyopangwa kufanyika Oktoba mwaka huu. Aidha, Balozi huyo mwenye makazi yake mjini Nairobi, Kenya, amesema kuwa kampuni moja ya Poland inawasiliana na Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) kuona kama inaweza kuwekeza katika uzalishaji wa magadi katika eneo la Ziwa Natron.

Katika mazungumzo yake na Balozi Julia Pataki wa Romani, Rais Kikwete amesifia uhusiano mzuri ambao sasa umefikisha miaka 50 kati ya Tanzania na Romania na kusema kuwa Tanzania imenufaika na uhusiano huo. “Katika miaka hii 50, tumeshirikiana kwa karibu sana. Mmetufundisha watu wengi katika nyanja mbali mbali na pia tumeshirikiana katika kuunga mkono mapambano ya ukombozi kusini mwa Afrika,” Rais amemwambia Balozi huyo mwenye makazi yake mjini Nairobi, Kenya.