Na Hassan Abbas, Addis Ababa
WAKATI Umoja wa Afrika (AU) ukitimiza miaka 50 na Mpango wa Afrika Kujitaghmini Kiutawala Bora (APRM) ukitimiza miaka 10, viongozi kadhaa waasisi Barani Afrika wametajwa kuwa mfano wa kuigwa.
Hayo yamebainishwa jijini hapa Jumatatu wakati wa ufunguzi wa mkutano wa siku mbili unaohusisha wataalamu wa masuala ya utawala bora kutoka sehemu mbalimbali Barani Afrika ulioandaliwa kuadhimisha miaka 10 ya APRM.
Wakizungumza katika mkutano huo wa siku mbili, unaotumiwa pia kama tafakuri ya utekelezaji wa malengo ya APRM, wachangiaji mbalimbali walieleza juu ya misingi adhimu ya utawala bora iliyowekwa na waasisi wa Bara hili akiwemo Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wa Tanzania.
Akifungua mkutano huo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa APRM Afrika, Assefa Shifaa, alimtaja Mwalimu Julius Nyerere, Rais wa zamani wa Msumbiji, Joachim Chissano na Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Mzee Nelson Mandela kuwa miongoni mwa viongozi walioenzi kivitendo dhana ya utawala bora kwa kuachia madaraka ya Urais wakati ambapo wananchi wao wengi bado walikuwa wakitaka waendelee kuongoza.
“Mwaka 1964 alipokuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hadi mwaka 1984 alipotangaza kung’atuka Nyerere na viongozi wengine wawili watatu wa Afrika waliokuja baadaye kama Mandela na Chissano walienzi misingi muhimu ya utawala bora kwa kuondoka madarakani kwa hiari, “alisema.
Katika hotuba yake Waziri Mkuu Dessalegn alisema chini ya Mpango wa APRM Bara la Afrika limeweza kuwashirikisha wananchi wake kutatua kwa pamoja na Serikali zao changamoto za msingi za utawala bora.
Alisema katika nchi 33 za Afrika zilizojiunga na APRM na ambapo nchi 17 ikiwemo Tanzania zimekwishakamilisha ripoti zao na ziko katika hatua za kuondoa changamoto zilizobainishwa, ni dalili kuwa Bara la Afrika limedhamiria kujinasua kutoka katika changamoto za utawala bora zinazolikwamisha Bara hilo.
Kwa upande wake, Rais Chissano naye alisifu jinsi demokrasia inavyokua Barani Afrika akisisitiza kuwa viongozi wengi kwa sasa wamekuwa tayari kutii matakwa ya katiba zao kwa kuondoka madarakani hivyo kupunguza mapinduzi ya kijeshi.
“Kutokana na kazi kubwa ya kuboresha utawala bora na demokrasia Afrika hivi sasa ni maoni yangu kuwa hata mapinduzi ya kijeshi yamepungua lakini pia viongozi wenyewe wa Afrika wamekuwa wakitii ukomo wa kikatiba wa uongozi wao,” alisema Rais Chissano akisisitiza kuwa viongozi wa Afrika wanapaswa kuitekeleza APRM kivitendo.
Sherehe za miaka 10 ya APRM zilizozinduliwa jijini hapa Jumatatu zinakwenda sambamba na shamrashamra za miaka 50 ya kuanzishwa kwa AU iliyoanzia na Umoja wa Nchi huru za Afrika (OAU)
APRM ni Mpango mahsusi wa Bara la Afrika ulioasisiwa mwaka 2003 kwa lengo la kutathmini utawala bora katika nchi kwa lengo la kuwashirikisha wananchi wenyewe na wadau wengine katika kubaini changamoto za kufanyiwakazi na mambo mazuri ili yaendelezwe.
Tanzania ilijiunga na APRM mwaka 2004, Bunge likaridhia kuanza kwa Mpango huo mwaka 2005 na shughuli za tathmini zikaanza mwaka 3008. Mpaka sasa Tanzania inasubiri kuanza utekelezaji wa Mpangokazi wa miaka mitano kuondoa changamoto zilizobaibishwa. Tathmini ya APRM hurudiwa kila baada ya miaka minne.