Sumbawanga
MWALIMU Mkuu wa Shule ya Msingi Chipu, Kata ya Kasense Manispaa ya Sumbawanga aweka poni Muhtasari wa masomo 13 kwa mfanyabiashara wa pombe na vinywaji baridi kwa ajili ya kuaminiwa na kisha kukopeshwa bidhaa hiyo.
Tuhuma hizo zimetolewa jana na mfanyabiashara maarufu, Singo Nzinyangwa anayemiliki duka la ‘Zawadi Store’ lililopo Manispaa ya Sumbawanga mjini.
Amesema mwalimu huyo Mkuu (jina tunalo) aliweka poni nyaraka hizo za masomo tangu Septemba Mwaka jana, baada ya kuchukua masanduku mawili ya bia na moja la soda, jambo ambalo linaathiri mwenendo wa biashara yake hadi sasa.
Nzinyangwa alitoa siri hiyo baada ya mteja wake mmoja kutaka kuaminiwa achukue bidhaa akiwa na fedha pungufu na baadaye angerejesha kiasi kilichopungua baada ya kufanya mauzo ya biashara yake.
Aidha Nzinyangwa aligoma kumuamini mteja huyo huku akimuonesha nyaraka hizo za shule ambazo zimetelekezwa na mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Chipu, baada ya kuaminiwa achukue bidhaa.
Baada ya mazungumzo hayo mfanyabiashara huyo alizitoa nyaraka hizo za shule na kuwaonesha baadhi ya wateja wake huku akisisitiza, hawezi kuwaamini kwani tayari ametendwa na baadhi yao kibiashara. “Haya oneni wenyewe vitu kama hivi ni vya walimu wameniachia baada ya kushindwa kulipa,” alisema Nzinyangwa.
Mfanyabiashara huyo alimuonesha mwandishi wa habari hizi nyaraka hizo, ambapo ni muhtasari wa TEHAMA nakala mbili, Hisabati nakala moja, Elimu ya Awali nakala tatu, Stadi za Kazi nakala moja, Historia nakala mbili, Kifaransa nakala moja, Kiingereza nakala moja, Haiba na Michezo nakala moja na nakala moja ya somo la Jiografia.
Aidha Nzinyangwa ambaye ni Mkurugenzi wa Zawadi Store alilithibitishia Jambo Leo kuwa ofisi yake inashikilia muhtasari ya masomo hayo kama poni kwa thamani ya sh. 90,000 kama thamani ya vinyaji vilivyochukuliwa na mwalimu Mkuu huyo.
Hata hivyo gazeti hili lilipomtafuta mwalimu huyo alikiri kuacha nyaraka hizo katika duka hilo na kudai alifanya hivyo baada ya kuzidiwa na mizigo mingi ya biashara siku hiyo na alidai aliyemuachia (Nzinyangwa) ni ndugu yake wa karibu.
Hata hivyo tayari Ofisa Mkaguzi wa Shule za Msingi Manispaa ya Sumbawanga, amemuamuru mwalimu huyo kulipa deni hilo la sh. 90,000 ili achukuwe nyaraka hizo mara moja kabla ya hatua kali kuchukuliwa dhidi yake.