WAKATI Serikali ikijaribu kupunguza adhabu za viboko kwa wanafunzi na kuweka mwongozo na utaratibu wa adhabu hizo, wananfunzi wanne wa Shule ya Sekondari Nsoho mkoani Mbeya wamejeruhiwa baada ya kuchapwa viboko 100 kila mmoja.
Tukio hilo linadaiwa kufanywa April 22 mwaka huu na mwalimu Lukindo Mwakanyasi,ambaye anafundisha shuleni hapo kwa mkataba.
Wakizungumza hivi karibuni kwa masharti ya kutotajwa majina, baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo wamesema wanafunzi waliojeruhiwa ni wa kidato cha kwanza, ambapo walipewa adhabu kabla ya mapumziko ya sikukuu ya Pasaka.
Wakifafanua zaidi walisema chanzo cha adhabu hiyo ni wanafunzi hao kudaiwa kumshutumu mwalimu huyo kuwa amekuwa na tabia ya kuwatongoza.
“Sisi tulishangaa siku hiyo wanafunzi wote wa kidato cha kwanza ‘A’ tuliamuliwa kutoka darasani majira ya saa 3:30 na kumuona Mwalimu Mwakanyasi na kuwaacha wenzetu wanne kisha kuanza kuwacharaza viboko,” alisema mmoja wanafunzi.
Alisema baada ya hapo walishuhudia wanafunzi hao waliokuwa wakichapwa wakitoka ndani ya darasa wakiwa wanalia kwa sauti za juu huku mashati yao yakiwa yamelowa damu.
Waliongeza kuwa baada ya hapo wanafunzi hao waliitwa katika ofisi ya Mkuu wa shule na muda mfupi ilikuja gari na hatimaye kuwachukuwa wanafunzi wawili ambao walionekana kujeruhiwa vibaya na fimbo za mwalimu huyo.
Mwandishi wa habari hizi alipofika shuleni kupata ufafanuzi wa tukio hilo, Mkuu wa shule hiyo, Violeth Bakaza alikataa kueleza chochote akidai kuwa yeye si msemaji.
“Jamani mimi mtanionea suala hili lipo kwa Ofisa elimu upande wa sekondari, mimi ninachokifanya nimelifikisha huko na nimeamuliwa kuandika taarifa kama mnavyoona naendelea nayo hivi sasa,” alisema kwa kifupi Bakaza.
Naye ofisa Elimu Mbeya,Joseph Shauri alipopigiwa simu alisema suala hilo lipo chini ya Mkurugenzi wa Halmashauri Mji wa huo, hivyo yeye asingeweza kulizungumzia.
Habari hii kwa hisani ya Gazeti la Jambo Leo, Dar es Salaam.