MVUA kubwa iliyonyesha kwa siku mbili mfululizo tangu juzi imesababisha vifo vya watu watano huku mamia wakikosa makazi baada ya nyumba zao kubomolewa. Mvua hiyo iliyofikia kipimo cha milimita 132.5 kwa mujibu wa vipimo vilivyofanywa katika kituo cha Shule ya Msingi ya Maktaba, ilisababisha barabara kujaa maji na nyingine kuharibika na madaraja kadhaa kukatika. Mkurugenzi Mkuu wa Hali ya Hewa, Dk Agnes Kijazi alisema jana kwamba kipimo hicho cha mvua ni cha juu mno kulinganisha na kile cha wastani ambacho ni kati ya milimita 16 na 30.
“Kwa takwimu za mwezi Mei, kiwango hiki hakijawahi kufikiwa kwa miaka 10 iliyopita.” Alipotakiwa kufafanua miezi mingine, Dk Kijazi alisema hakuwa na takwimu kwa kuwa alikuwa nje ya ofisi.
Awali, Dk Kijazi alitoa taarifa ikisema mifumo ya hali ya hewa inaonyesha kuwa “hali ya mvua inatarajiwa kuendelea katika baadhi ya siku hadi Mei 20, mwaka huu”.
“Mamlaka inaendelea kushauri wakazi wa maeneo hatarishi pamoja na watumiaji wa bahari kuchukua tahadhari,” alisema Dk Kijazi.
Watano wafa
Kutokana na mafuriko hayo, watu watano wakiwamo watoto wawili, walipoteza maisha baada ya kusombwa na maji. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick alisema waliopoteza maisha ni watoto wawili na mzee mmoja ambao majina yao hayajafahamika.
“Mtoto mmoja (2) alisombwa na mafuriko katika eneo Machimbo ya Makangarawe na mzee mmoja alifariki jana baada ya mvua kunyesha na kujaa ndani ya nyumba yake. Mtoto mwingine ambaye bado hajapatikana alisombwa na mafuriko pia,” alisema Sadick.
Hata hivyo, habari zilizopatikana wakati tunakwenda mitamboni zilisema kuwa waliopoteza maisha ni watu watano.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alimtaja mtu aliyefariki dunia kuwa ni Shabani Idd (73) mkazi wa Manzese. Katika eneo la Mbezi Luis, Mto Mbezi ulifurika, hali iliyosababisha nyumba zilizojengwa kandokando ya daraja hilo kufunikwa na maji.
Mkazi wa eneo hilo, John David alisema hali ilikuwa mbaya zaidi jana asubuhi kwani maji yalifurika na kujaa barabarani na kusababisha usumbufu mkubwa kwa watumiaji. Alisema wakazi walio karibu na mto huo walichukua tahadhari tangu juzi na kuhama makazi yao.
“Haikuwa rahisi kwa wao kuendelea kukaa hapa wakati wanafahamu hali kama hii ingetokea. Tangu jana jioni familia zinazoishi huko ziliondoka, lakini vitu vyao vimesombwa na maji na nyumba moja imesombwa pia,” alisema David.
Maeneo ya Boko Basihaya, zaidi ya nyumba 20 zilikuwa zimezingirwa na maji huku familia kadhaa zikilazimika kukimbia nyumba zao na kutafuta makazi ya muda kuanzia juzi usiku hadi jana.
Timu ya waandishi wa Mwananchi ilifika katika eneo hilo na kushuhudia maji yakiwa yamejaa kwenye nyumba zilizojengwa kandokando ya bwawa linalotiririsha maji kuelekea baharini. Mmoja wa wakazi wa eneo hilo, Dionise Swai alisema baada ya maji kujaa nyumbani kwake, alilazimika kuyanyonya kwa kutumia pampu ili kunusuru mali zake.
“Niliyawahi kwa hiyo hayakuingia. Wanafamilia wengine wameondoka nimebaki mwenyewe,” alisema.
Mkazi wa mwingine eneo hilo, Frank Shuma alizitupia lawama mamlaka kwa kushindwa kujenga mifereji ya kutiririsha maji kwenda baharini. Hali kama hiyo pia ilitokea eneo la Kinondoni Hananasif ambako maji yalijaa na kufunika baadhi ya nyumba.
Katika daraja la Kawe, wananchi walikuwa kwenye harakati za kuokoa mali zao zilizosombwa na maji, yakiwamo magodoro, vyombo na nguo. Maji yalijaa kwenye barabara na kusababisha vyombo vya moto na watembea kwa miguu kupita kwa shida huku magari mengine yakilazimika kusimama pembeni.
Barabara ya Haile Selassie, upande wa baharini karibu na Hoteli ya Sea Cliff, eneo hilo lilifunikwa na maji na kusababisha usumbufu kwa vyombo vya moto na madereva kulazimika kuendesha kwa mwendo wa taratibu na kusababisha foleni.
Watumiaji wa barabara ya Mwai Kibaki walikuwa na wakati mgumu kupita, wengi walionekana wakiwa wamevua viatu au kutafuta njia mbadala kukwepa maji yaliyokuwa yamejaa barabarani. Mkazi wa Ubungo Kibangu, Julieth Kibakaya alisema hofu imetanda kwa wakazi wa eneo hilo kutokana na athari zinazosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha hasa mafuriko.
“Huku kwetu hali ni mbaya. Mafuriko yamebomoa nyumba mbili hadi sasa. Hivi sasa wanafamilia hao hawana makazi tena imebidi wapewe hifadhi ya muda na majirani zao na hali ikiendelea hivi tunahofia wakazi wengi wa eneo hili watapoteza nyumba zao,” alisema Kibakaya.
CHANZO: Gazeti Mwananchi