Na Joachim Mushi
MVUA kumbwa iliyonyesha usiku wa kuamkia leo maeneo kadhaa ya Jiji la Dar es Salaam imeleta maafa makubwa, ikiwemo kuua, kubomoa baadhi ya majengo na kuharibu mali mbalimbali za wananchi.
Mvua hizo zilizonyesha zaidi pembezoni mwa Jiji la Dar es Salaam zimesababisha baadhi ya barabara za jiji kushindwa kupitika kwa muda baada ya madaraja kuziba na maji kupita juu ya madaraja hao hivyo magari kushindwa kupita.
Thehabari imetembelea maeneo kadhaa ambayo yameathiriwa na mvua hiyo na kushuhudia uharibifu mkubwa na hasara imeosabaishwa na mvua hizo. Maeneo ya Sinza-Kamanyola jirani na Shule ya Msingi/Sekondari Mugabe baadhi ya majengo zikiwemo; baa, nyumba na maduka yameharibiwa vibaya.
Maji ya mvua yaliyokuwa yakitiririka yamebomoa na kusomba mali mbalimbali kwenye baadhi ya maduka, baa na nyumba za watu. dev.kisakuzi.com imeshuhudia gari dogo aina ya Suzuki likiwa limesombwa na maji na kupelekwa bondeni pembezoni mwa mfereji mkubwa unaopitisha maji machafu katika daraja la Shekilango, Sinza.
Magari yalishindwa kuvuka daraja la bonde la Shekilango, jirani na eneo la Kamanyola baada ya daraja hilo kujaa maji na kufunika daraja zima kuanzia majira ya saa kumi na moya asubuhi hadi saa moja asubuhi. Maji hayo pia yalikosa mwelekeo na kuanza kuingia kwenye maduka, baa na nyumba za watu maeneo jirani na daraja hilo hivyo kubomoa kuta na kuharibu mali kadhaa.
“Maji yalikuwa yamejaa eneo lote kuanzia kituo cha daladala cha Kamanyola (Sinza) hadi darajani ukielekea Shekilango, magari yalishindwa kupita…baadhi ya vitu vimeshombwa na maji baada ya kuingia ndani,” alisema mmoja wa shuhuda ambaye hakujitambulisha.
Akizungumza na dev.kisakuzi.com Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Kwatumbo-Tandale, Zinduna Tumbonaga (CCM) amesema kikosi cha uokoaji kutoka ‘fire’ kimeokota maiti ya kichanga eneo hilo ambayo ilizolewa na maji. Hata hivyo haikuweza kufahamika kichanga hicho kilisombwa eneo gani ama mama wa mtoto alijifungua na kukitupa kwenye maji.
Tumbonage amesema mama mmoja amevunjika mguu kutokana na maafa hayo, maji yameingia katika nyumba nyingi za wakazi wa eneo hilo huku baadhi ya watu wakishuhudia mali zao zikisombwa na maji. Barabara ya Tandale kuanzia Daraja la TP Afrika ilikuwa imejaa maji na haipitiki hadi mbele ya eneo la Kwatumbo hivyo kuleta usumbufu mkubwa.
“Kila mtu aliangalia kwanza usalama wake na watoto mali ilikuwa ni baadaye, watu wameanza kuangalia mali baada ya maji kupungua…eneo hili vibaka walijifanya waokoaji hivyo kutoweka na mali za baadhi ya watu,” alisema mmoja wa wafanyabiashara pembezoni mwa barabara ya Tandale.
Taarifa zinasema kwamba eneo la TP Afrika imeokotwa maiti ya mzee (babu) ambayo inasadikika ilikuwa ikisombwa na maji. Haikujulikana mara moja kifo hicho kilitokea umbali gani kutokana na maji kutiririka kutoka mbali. Baadhi ya familia zimelazimika kukimbia maeneo yao na hata wazazi kuhamisha watoto wao kwenda maeneo yenye usalama.
Thehabari.com imeshuhudia wananchi wakitoa maji, matope na taka mbalimbali ndani ya nyumba, maduka na baa zilizojaa maji na kufanya uharibifu mkubwa. Maeneo yaliozidiwa na maji ni Tandale –Kwatumbo na Mkunduge, Uwanja wa TP Afrika na nyumba za jirani na uwanja huo, Sinza Kamanyola, Bonde la Msimbazi-Kigogo, Mburahati, Mabonde yote ya Barabara ya Kawawa.
Jeshi la Polisi limelazimika kutumia helikopta kukagua baadhi ya maeneo yalioathirika zaidi na mvua hizo tangu asubuhi ili kuangalia namna ya kutoa msaada maeneo yanayohitaji. Helikopta tatu zilionekana zikizunguka maeneo mbalimbali ya Jiji kuangalia usalama kwa waathiriwa na maafa hayo.