Mvua zaathiri makazi ya muda ya waathirika Gongo la Mboto

HALI ni mbaya kwa familia zilizoathirika na milipuko ya mabomu kwenye kambi ya Jeshi la Wananchi nchini (JWTZ), kikosi cha 511 Gongo la Mboto Dar es Salaam na sasa familia hizo zimelazimika kuyakimbia makazi ya muda ya mahema baada ya kujaa maji.

Hali hiyo imetokea jana baada ya mvua kubwa kunyesha eneo la Gongo la Mboto na maji kuanza kuingia kwenye mahema ya muda waliojengewa kujihifadhi baada ya nyumba zao kubomolewa na milipuko ya mabomu ya hivi karibuni.

Mvua hizo zilizoanza kunyesha majira ya saa saba mchana jana zimeziathiri zaidi ya familia saba maeneo ya Majohe na zililazimika kuanza kuhamisha vitu ambavyo vilivyokuwa vikilowa ndani ya mahema yao.

Akizungumza na mwandishi wa habari hii mmoja wa wanafamilia mkazi wa Majohe anayeishi kwenye mahema hayo, Manka Mushi alisema wamelazimika kuyakimbia makazi yao kwa muda huku mvua ikinyesha baada ya maji ya mvua hiyo kubwa kuanza kuingia ndani.

“Mvua bado inaendelea kunyesha baadhi ya vitu na hasa misaada yetu tuliopewa na wasamaria imelowa…tumelazimika kuhamisha baadhi ya vitu ili visiendelee kuharibiwa na maji ya mvua. Jamani tunaombeni msaada maji yanaingia ndani ya mahema yetu,” alisema Mushi akizungumza na mwandishi wa habari hii.

Alisema kuna kila sababu ya mamlaka husika kuangalia namna ya kuwasaidi juu ya suala hilo kwani endapo mvua zitaendelea kunyesha kama ilivyotokea, na hasa kunyesha usiku huenda ikaleta usumbufu na madhara makubwa kwa familia zilizopewa hifadhi kwenye mahema.

Hata hivyo mwandishi alipozungumza na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Leonidas Gama alikiri kupokea taarifa kuwa mvua zilizonyesha zimeleta usumbufu kwa baadhi ya familia kwani, wamepata taafifa kuwa maji yalikuwa yakiingia ndani ya mahema.

“Ni kweli tumepokea taarifa kuwa kuna mvua zinanyesha maeneo ya Majohe na familia ambazo zilikuwa zimejihifadhi kwenye mahema maji yalikuwa yakiingia ndani ya mahema kupitia juu…tayari tumetuma timu ya watu wa Msalaba Mwekundu kuangalia nini tatizo,” alisema Gama akizungumza kwa njia ya simu jana.

Alisema alipokea taarifa kutoka katika familia mbili maeneo ya Majohe zikiripoti tatizo hilo, ambapo muda mfupi aliwaarifu kikosi cha Msalaba Mwekundu kwenda kuchunguza tatizo na kuangalia nini cha kufanya ili kuondoa adha hiyo.

Milipuko hiyo ya mabomu iliathiri nyumba 69, zenye familia 119 zikiwa na idadi ya watu 459. Jumla ya vifo vilivyosababishwa na milipuko hiyo ni 29 hadi sasa. Tayari Serikali imetangaza kulipa kifuta machozi kwa familia zilizofiwa, ambapo kila mfiwa atapewa kiasi cha sh milioni 8.5.

Mwisho.