Na Joachim Mushi, Dar es Salaam
MVUA iliyonyesha mfululisho tangu jana maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam imeleta patashika kwa baadhi ya maeneo ikiwemo kufunika nyumba na kusomba baadhi ya mali za wananchi na watu jambo lililozua hofu na kero kwa wakazi wengi wa jiji hasa wale wanaoishi maeneo ya mabondeni.
Maeneo ya Bonde la Mto Msimbazi baadhi ya nyumba zimefunikwa na maji usawa wa madirisha na maji kusomba mali za wakazi wa maeneo hayo pamoja na kusababisha maafa makubwa ikiwemo baadhi ya watu kupotea jambo ambalo limezua hofu kubwa. Uchunguzi uliofanywa na mtandao huu maeneo ya Jangwani, Tabata, Kigogo yote yanayopitiwa na Bonde la Mto Msimbazi na maeneo ya Mbagala Kizinga hali ni mbaya zaidi tangu jana usiku.
Mwandishi wa habari hizi ameshuhudia baadhi ya wananchi maeneo ya Kigogo Mjimpya maarufu kwa ‘Dua Said’ maji yakiwa yamefunika baadhi ya nyumba na zingine zikiwa zimejaa maji usawa wa madilisha huku wananchi wakijitahidi kuokoa baadhi ya mali zao ilhali mvua hiyo ikiendelea kunyesha mfululizo.
Eneo la Magomeni Jangwani katika Barabara ya Morogoro majira ya mchana leo kipande cha barabara hiyo kililazimika kufungwa baada ya maji kujaa eneo hilo na kufunika barabara hiyo kabisa. Askari Polisi walilazimika kuzuia magari kuendelea kupita eneo hilo kwa kuhofia madhara zaidi. Daladala zinazotumia barabara hiyo zinazofanya safari ya Mwenge – Kariakoo na Ubungo-Kariakoo zililazimika kutumia barabara ya Kawawa kwa muda kutokana na hali hiyo. Baadhi ya daladala zimepandisha bei nauli hivyo kuleta usumbufu na kero kwa wananchi.
Maeneo ya Tabata Bonde la Mto Msimbazi nyumba zilionekana kuvamiwa na maji huku baadhi ya familia zikilalamika kupoteza baadhi ya wanandugu wakiwemo watoto na watu wazima na mali zao kadhaa. Vyombo vimesobwa na maji na kuwalazimu wakazi kupanda juu ya nyumba na maeneo ya miinuko kujinusuru na hali hiyo ya maafa.
“…Kuna baadhi ya familia zinalalamika kupoteza watoto tangu jana usiku walipokuwa wakikimbia maji katika nyumba zao, sasa haijulikani kama wamesombwa na maji au wapo salama lakini wamekimbia maji…,” alisema mama mmoja mkazi wa eneo la mji mpya bonde la mto Msimbazi Tabata akizungumza na mwandishi wa habari hizi.
Mwandishi wa habari hizi alishuhudia baadhi ya vitu vilivyosombwa na maji vikipita katika Mto Msimbazi eneo la Tabata Matumbi na Bonde la Mto Msimbazi eneo la Kigogo, huku baadhi ya vijana wakiviopoa vitu hivyo vikiwemo viti, mbao za vitanda na kutoweka navyo kusiko julikana.
Maeneo ya Tabata Kizinga hali ilikuwa mbaya baada ya baadhi ya nyumba kufunikwa na maji na kusomba vitu anuai huku familia za maeneo hayo zikijinusuru kwa kupanda juu ya mapaa. Familia nyingine zilionekana kujitahidi kuokoa baadhi ya vifaa huku mvua ikiendelea kujaa. Maeneo ya barabara ya Mandela jirani na Tabata Matumbi maji yalifunika barabara hiyo kwa muda na kuzua foleni kubwa ya magari tangu jana usiku hivyo kuleta usumbufu kwa watumiaji wa barabara hiyo.
Baadhi ya maeneo ya Msasani nayo yalifurika maji na baadhi ya nyumba kuvamiwa na maji hadi ndani jambo ambalo limewalazimu wakazi wa nyumba hizo kuzikimbia. Barabara ya Msasani imelazimika kufungwa baada ya maji kuiharibu vibaya baadhi ya maeneo hivyo kushindwa kupitika kirahisi.
Hata hivyo mvua bado inaendelea kunyesha mfululizo karibuni maeneo yote ya jiji la Dar es Salaam, jambo ambalo imefanya baadhi ya maeneo kujaa maji na kufunga barabara za mitaa hiyo na kuleta usumbufu kwa watumiaji. Hadi tunakwenda mitamboni mvua bado imeendelea kunyesha mfululizo.
Baadhi ya viwada vilivyopo pembezoni mwa Mto Msimbazi eneo la Tabata Matumbi, katika Barabara ya Mandela tangu jana usiku vililazimika kusimamisha shughuli za uzalishaji baada ya maji kuvunja kuta za ukingo na kuingia eneo la ndani ya viwanda hivyo. Wafanyakazi wa viwanda hivyo waliacha shughuli za uokoaji na kuanza kupambana na maji kwa kutoa baadhi ya vifaa na mali ili zisiharibiwe na maji yaliyoingia eneo la viwanda hivyo. Inaelezwa kuwa mvua hizi pia zimesababisha baadhi ya ndege kushindwa kutua katika Uwanja wa Kimataifa wa Julias Nyerere na ndege hizo kutua viwanja vya nchi jirani kutokana na baadhi ya maeneo ya uwanja huo kujaa maji.
Hadi tunaripoti taarifa hizi mamlaka husika bado hazijataja kama mvua hizi zimesababisha baadhi ya watu kupoteza maisha na wala kujua kiasi cha madhara kilichosababishwa na mvua hizi.
Tayari tahadhari imetolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini, TMA tangu juzi kuwa zitanyesha mvua kubwa na zinaweza kuleta madhara hivyo kuwataka wananchi kuchukua tahadhari hasa wale wakazi wa mabondeni. Maeneo yaliotajwa kwenye taarifa ya TMA kuwa yatakuwa na mvua nyingi ni pamoja na Visiwa vya Unguja na Pemba, mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga, na upo uwezekano wa mvua hizo kusambaa katika mikoa ya Lindi, Mtwara na Morogoro.
Taarifa ya TMA imeeleza kuwa hali hiyo inatokana na kuimarika zaidi kwa ukanda wa mvua “Inter-tropical convergence zone (ITCZ)” ambao umeambatana na ongezeko la unyevunyevu katika eneo la bahari ya Hindi. Imeeleza kuwa mvua hizo zitaendelea hadi Aprili 14 katika maeneo tajwa. TMA imevitaka vikosi na mamlaka ya uokoaji kuchukua tahadhari kutokana na hali hiyo.
Mtandao huu unaendelea kufuatilia na utatoa taarifa kadri zinavyotufikia.