Mvua ya Samaki Yanyesha Kijijini

Mvua ya Samaki ikinyesha  Sri Lanka.

Mvua ya Samaki ikinyesha Sri Lanka.

WAKAZI wa kijiji kimoja Magharibi mwa Sri Lanka wameshangazwa na pia kwa namna nyingine kufurahishwa na tukio la ‘kunyesha’ kwa mvua ya Samaki wadogo kijijini kwao. Samaki hao ambao walikuwa katika hali nzuri ya kuweza kulika wanaaminika kuwa walibebwa kutoka kwenye mto mmoja kwa upepo mkali na kuangukia kijijini hapo.

Wanakijiji hao wa Wilaya ya Chilaw walisema walisikia kitu kizito kikianguka na baada ya kutizama wakaona ni samaki wengi wenye uzani wa kilo hamsini. Hili si tukio la kwanza la aina hii kuwahi kutokea Sri Lanka, kwani mwaka 2012, kulitokea kisa cha mvua ya viumbe vya baharini vijulikanavyo kama ‘Kamba’ ambavyo huliwa pia na watu.

Wanasayansi wanasema kuwa mvua ya Samaki hutokea wakati ambapo upepo mkali unavuma juu ya maji ya kina kifupi na hivyo kusababisha mzunguko wa maji unaovuta karibu kila kitu kilicho ndani ya maji ikiwa ni pamoja na samaki na hata vyura na kuwaangushia maeneo mengine.

Viumbe hawa wa majini wanaweza wakasafirishwa kwa masafa marefu kwa kushikiliwa na mawingu hata baada ya ule mzunguko wa maji kuisha. Wanakijiji walisema kuwa mvua hiyo ya Samaki ilinyesha Jumatatu huku viumbe wale wakianguka kwenye mashamba, barabarani na paa za kijiji hicho.

Baadhi ya samaki hao wenye urefu wa kati ya sentimita tano na nane, walikuwa bado wako hai na walitiwa kwenye ndoo za maji na wanakijiji waliowatumia kama kitoweo badaye. Hii ni mara ya tatu kwa tukio kama hili kufanyika Sri Lanka, ingawa katika eneo tofauti.

Kando na ile mvua ya ‘Prawn’ya mwaka wa 2012 kusini mwa Sri Lanka, mvua ya kimondo (meteors) nyekundu na manjano ilinyesha mwaka huo huo,tukio ambalo bado linachunguzwa na wanasayansi wa Marekani na Uingereza.

-BBC