MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema mvua kubwa zinatarajia kunyesha tena Aprili 17 na 18 katika Visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na mikoa ya Tanga, Pwani na Dar es Salaam. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari, mvua hizo zinatarajiwa kunyesha katika kipimo kinachozidi milimita 50 ndani ya saa 24, katika Ukanda wa Pwani.
TMA imewataka wakazi wa maeneo hatarishi yaliotajwa, watumiaji wa Bahari pamoja na mamlaka zinazohusika na maafa, kuhakikisha wanachukua tahadhari stahiki ili kuweza kukabiliana na majanga yoyote yanayoweza kusababishwa na mvua hizo.
Taarifa hiyo imefafanua kuwa hali hiyo inatokana na kuimarika kwa ukanda wa mvua “Inter-tropical convergence zone (ITCZ)” ambao umeambatana na ongezeko la unyevunyevu na kuwepo kwa ‘Easterly Wave’.
“…Mamlaka ya Hali ya Hewa inaendelea kufuatilia hali hii na itatoa mrejeo kila itakapobidi.
Imetolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania,” alisema katika taarifa yake.