MUVI yaanza kutoa elimu kwa wakulima Njombe

Wakulima Njombe wakisoma baadhi ya majarida na vipeperushi juu ya elimu ya kijasiriamali walipotembelewa na MUVI.

Na William Macha, Njombe

MRADI wa Muunganisho wa Wajasiriamali Vivijini (MUVI) kupitia kitengo chake cha habari umeingia Njombe na kufanikiwa kuzungumza na wajasiriamali wa zao la nyanya na alizeti kutoka mkoani humo. Katika hatua ya kwanza kitengo hicho cha habari kimefanya ziara kwenye vijiji vya Igongolwa, Lyamkena, Ikwete, Kiumba, Itipingi, Ibiki, Mahongole, Kifumbe, Uselule na Imalinyi.

Wajasiriamali kutoka katika vijiji hivyo wamepatiwa elimu ya uzalishaji bora pamoja na masoko huku changamoto kubwa ikibakia kuwa ni usafirishaji wa bidhaa zao (nyanya) hizo kutoka shambani kuelekea sokoni.

Wakielezea matatizo wanayokumbana nayo katika uzalishaji wa nyanya wakulima hao wamesema kuwa ni ukosefu pembejeo za kilimo, mitaji na miundombinu ambayo huwazuia wanunuzi kufika katika maeneo ya karibu kununua nyanya.

“Tunasafiri umbali mrefu kupeleka nyanya hususani sisi wanakijiji wa Igongolo, tunakokota baiskeli ikiwa na nyanya umbali wa zaidi ya kilometa 10 tunafika sokoni tukiwa tayari tumechoka sana hali ambayo huwafanya wanunuzi kutumia uchovu wetu kutugandamiza,” alisema Kasimu Timbuka kutoka katika kikundi cha Songambele.

Aidha wanakijiji hao wameiomba MUVI iwahimize viongozi wa ngazi mbalimbali serikalini wawaboreshee miundombinu ili usafirishaji wa bidhaa zao kutoka shambani hadi sokoni uwe rahisi. Pamoja na hayo mradi wa MUVI imewataka wakulima kutoka vijiji hivyo kupanda mbegu bora za nyanya katika msimu huu ambao tayari shughuli za upandaji zimeanza.

Kuhusu mitaji MUVI tayari imewaunganisha wajasiriamali katika vikundi na tayari vikundi zaidi ya 90 kutoka katika vijiji 30 vimeundwa. Vikundi hivi vitawasaidia wajasiriamali kupata mikopo kutoka asasi mbalimbali za kifedha hapa nchini.

Katika upande mwingine wanakikundi kutoka katika Kijiji cha Mahongole wameahidiwa kujengewa soko la kuuzia nyanya zao na mradi wa Muunganisho ujasiriamali vijiji huko taratibu za ushawishi zikiendelea ili kuweza kuwasaidia wanaokabiliwa na tatizo la soko la kuuzia nyanya.

Wakulima wa nyanya na alizeti mkoani humo watakuwa wakipatiwa taarifa za uzalishaji pamoja na masoko kupitia kitengo cha habari mkoa pamoja na kituo cha Redio cha Upland FM.