Na Mwandishi wa dev.kisakuzi.com, Dodoma
HATIMAYE Bunge limepitisha muswada wa Sheria wa Kuunda Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambao hata hivyo wabunge wa vyama vya upinzani vya CHADEMA na NCCR-Mageuzi waligoma kuujadili na kutoka nje ya Bunge hadi jana ulipopitishwa.
Hatua ya kupitishwa kwa muswada huo ilifikiwa jana baada ya Spika wa Bunge, Anne Makinda kuwahoji wabunge hatua ya kupitisha ama kutopitisha muswada huo. Wabunge wengi walioujadili na hata kuupitisha ni wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) pamoja na Chama cha Wananchi-CUF.
Muswada wa Kuunda Tume ya Kukusanya Maoni uliopitishwa jana na Bunge kwa sasa unasuburi kusainiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano kabla ya kuwa sheria rasmi na kuanza kutumika mara moja.
Awali akizungumza, Spika Makinda alisema kitendo cha baada ya wabunge wa upinzani kutoka nje ya Bunge kukwepa mjadala wa muswada huo, wamewanyima haki wanaowawakilisha kuweza kuchangia maeneo mbalimbali.
Tayari Chama cha CHADEMA kimetoa tamko la kupinga hatua ya kupitishwa kwa muswada huo kuwa sheria na kudai waliopitisha si wabunge bali ni wana-CCM hivyo wananchi wasiutambue na wao wanajiandaa kuwasilisha muswada mwingine.
Hata hivyo wanaharakati na baadhi ya makundi yapepanga kufanya maandamano nchi zima chini ya Jukwaa la Katiba kupinga hatua hiyo ya Bunge kupitisha muswada ambao ulikuwa na utata.