Museveni Awapongeza Mwalimu Nyerere, Karume

Hayati, Julias Kambarage Nyerere

Na Mtuwa Salira, EANA

RAIS Yoweri Museveni wa Uganda amewaelezea viongozi waanzilishi wa taifa la Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere na Shekhe Abeid Karume kuwa walikuwa viongozi wenye muono wa hali juu katika Afrika Mashariki walioacha ubinafsi wa mamlaka ya nchi zao na kuunganisha watu wao kwa lengo la kuwa na umoja imara.

“Viongozi hao wanastahili kutambuliwa kwa maamuzi yao ya busara ya kuunganisha Tanganyika na Zanzibar kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” Rais Museveni aliwaambia wajumbe wa semina ya mahusiano ya wabunge mjini Entebe, Uganda mwishoni mwa wiki.

Hatua hiyo ya kishujaa na ya kupongezwa haina budi kuigwa na nchi wananchama wa Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC), aliongeza, Shirika Huru la Habari la Afrika Mashariki (EANA) linaripoti.

Nyerere alistaafu urais mwaka 1985 na kufariki mjini London Uingereza Oktoba 14, 1999 akiwa na umri wa miaka 77. Shekhe Karume (67) aliuawa Aprili 1972 mjini Zanzibar.

Rais Muveni alikuwa anahutubia semina ya siku mbili yenye kauli mbiu : “Kukuza soko lenye misingi ya watu wa Afrika Mashariki.”

“Huku ikiwa na idadi ya watu milioni 140, Afrika Mashariki ina soko kubwa ambalo linaweza kuvutia kwa urahisi wawekezaji ambao wanaweza kujenga viwanda katika kanda hii,” Museveni alitoa maoni yake juu ya kauli mbio hiyo, kwa mujibu wa gazeti la Monitor la nchini Uganda.

Aliongeza: “Ubaguzi unaotokana na tofauti za kikabila na dini zinapingana na matakwa ya wote, wazalishaji na wafanyabishara.”

Alitoa changamoto kwamba kuunganishwa kwa Afrika Mashariki ilikuwa “ni lazima kwa kuwa watu katika kanda hiyo walikuwa tayari wameunganishwa kwa utamaduni na lugha zao.”