Multiple Myeloma Muuaji wa Kimyakimya Tanzania

Dkt. Sanjay

KILA MWAKA kesi mpya zinazohusiana na ugonjwa wa saratani huripotiwa kuwa chanzo kikuu cha vifo vingi nchini Tanzania. Wataalamu wanatabiri hatua madhubuti zisipochukuliwa mapema kukabiliana na ugonjwa wa saratani, kutakuwa na ongezeko kubwa la vifo vitokanavyo na ugonjwa huo.
Kulingana na utafiti uliofanyika hivi karibuni juu ya magonjwa ya saratani unaonyesha kuwa, saratani ya mapafu na saratani ya kinywa ndizo saratani zinazoongoza kwa wanaume wakati wanawake hushambuliwa zaidi na saratani ya kizazi na saratani ya maziwa.
Ongezeko kubwa la magonjwa yanayohuisishwa na aina mbali mbali za saratani katika nchi maskini na zinazoendelea, imepelekea msukumo kwa Hospitali za Apollo; Hyderabad na kuifanya ichukue hatua za kutoa elimu za aina kadha wa kadha za saratani ikiwemo aina ya saratani iitwayo Multiple Myeloma. Ambayo ni aina ya saratani isiyofahamika miongoni mwa watu wengi lakini ni hatari.
“Ukosefu wa vifaa maalumu vya matibabu na uelewa mdogo nchini Tanzania ndivyo vimepelekea ungonjwa wa kansa kuwa hatari zaidi. Lakini ukweli ni kwamba mgonjwa wa kansa akigunduliwa mapema, basi anaweza kupata tiba na kupona na kuendesha maisha bora,” anazungumza Dkt. Sanjay Maitra kutoka Hospitali za Apollo, Hyderabad.
Uchunguzi aliofanyiwa mtanzania Dkt. Philip Robert Hiza hivi karibuni katika hospitali ya Apollo nchini India, aligundulika kuwa na saratani ya Multiple Myeloma. Ambako alilazwa na kufanyiwa matibabu kwa miezi mitano.
Katika jitihada za kukabiliana na aina hii ya saratani zinazofanywa na Hospitali za Apollo, hospitali hiyo ya kimataifa ilileta wataalamu wake nchini Tanzania ili kufanya vipindi vya uchunguzi na kuwashauri wagonjwa wenye aina hiyo ya saratani. Moja kati ya wagonjwa waliofika katika vipindi hivyo ni Dr. Hiza ambaye kwa sasa anaendelea kupata ahueni baada ya matibabu ya muda mrefu.

Saratani ya multiple myeloma inayojulikana pia kama seli za damu za myeloma, ni aina ya saratani ya seli za damu ( chembe chembe nyeupe za damu zinazotengeneza kingamwili) inayoanzia kwenye uboho (bone marrow). Katika saratani ya myeloma, seli za damu zinapoharibika hujikusanya kwenye uboho(bone marrow) na kutengeneza protini mbovu zinazotengeneza uvimbe na kuingilia mfumo wa utengenezaji wa seli za damu zinazosaidia kulinda mwili dhidi ya maradhi. Seli mbovu za myeloma husambaa kwa makundi makubwa katika mfumo wa damu mwilini hivyo kupelekea kuundwa kwa multiple myeloma ambazo hushambulia chembe chembe hai za damu (aina ya chembe hai za damu zinazohusika na kutengeneza antibodies).
Ni jukumu la kila mtu katika jamii zetu kupambana na majanga kama haya yanayozonga jamii zetu kwani katika miaka 10 iliyopita, njia za matibabu ya ungonjwa wa Multiple Myeloma zimeongezeka na kupelekea ahueni kwa wagonjwa wa aina hiyo ya saratani linaripoti shirika moja la Multiple Myeloma Research Foundation (MMRF) lililoko nchini Marekani (i). Jambo ambalo linaunga mkono jitahada zinazofanywa na Hospitali za Apollo.
Taswira iliyotolewa mwaka 2012 na mashirika ya kimataifa ya GLOBOCAN na International Agency for Research on Cancer – WHO inakadiriwa kuwa katika Afrika ya Mashariki pekee kunaripotiwa kesi 1832(0.6%) za watu wenye saratani ya myeloma, vifo vya watu 1621(0.8%) na 2726(0.5%) asilimia ya kuenea kwa saratani ya myeloma.
Hali kadhalika vyanzo mbali mbali vya habari vinaonyesha kwamba wanaume ndio wanaoongoza kwa kugundulika na saratani ya multiple myeloma kuliko wanawake kutokana na sababu zisizofahamika. Kulingana na data hizi, katika Afrika ya Mashariki idadi 863(0.7%) ya wanaume waligundulika na saratani ya hiyo ikisababisha vifo 765(0.8%) vya wanaume na 1327(0.7%) ya uneaji wa saratani hiyo miongoni mwa wanaume. Kwa upande mwingine wanawake 969(0.6%) waliripotiwa kuwa na saratani hii ikisababisha vifo vya wanawake 856(0.7%) na ueneaji miongoni mwa jinsia hiyo katika idadi ya 1399(0.4%) (ii).
Wataalamu hawajafanikiwa kugundua nini haswa husababisha saratani ya myeloma lakini kuna nadharia kadhaa zinazopelekea saratani hiyo kama kuwa kwenye mazingira hatarishi ya madawa ya kuulia wadudu,madawa ya kupulizia kwenye mimea, benzini, rangi za nywele na mionzi yanayokisiwa kuchangia kuugua saratani ya myeloma. Pia, hakuna ushahidi wowote kuhusu saratani hii kurithishwa kijenetiki.
Dalili kuu za ungonjwa ni pamoja na upungufu wa damu mwilini, kuvuja damu, maumivu makali, uchovu, figo kutofanya kazi, maambukizo na kuharibika kwa neva.
Hakuna vigezo hatarishi kwa wangonjwa wa saratani ya multiple myeloma kwani hutofautiana kwa baadhi ya wagonjwa. Vigezo hivo ni pamoja na umri ambapo watu wenye umri kati ya miaka 50 hadi 60 ndio wanaogundulika kuwa na saratani ya aina hiyo wakati kesi chache zikiripotiwa kwa watu wenye umri chini ya miaka 40. Wanaume ndiyo kundi lililo kwenye hatari zaidi ya kupata saratani ya myeloma kuliko wanawake. Watu wanene au wenye mafuta mengi mwilini wako pia kwenye hatari kubwa ya kuugua saratani hii pamoja na watu wanaofanya kazi au kuishi maeneo yenye mafuta ya petroli.
Kama ilivyoada kwa maisha ya mwanadamu kuwa na tumaini katika kila jambo, Hospitali za Apollo zinategemea kuanziasha kutoa huduma zinazohusiana na magonjwa ya saratani nchini Tanzania. Huduma hizo ni pamoja na uchunguzi wa kina, vipimo vya mkojo na damu na x-ray. Kutokana na kuwa na teknolojia za hali ya chini katika sekta ya afya nchini, ugonjwa wa Multiple Myeloma hauna tiba mbadala. Hivyo ujio wa wataalamu na teknolijia za kisasa za matibabu nchini kutasaidia kuboresha hali zorota inayosababishwa na magonjwa yasiyoambukizwa au magonjwa yanayosababishwa na mwenendo wa maisha.