Katibu Mkuu wa CCM, Willson Mukama
Dodoma,
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Willison Mukama amekiponda chama chake kwa kusema viongozi wengi ndani ya chama hicho ni ‘waroho’ (tamaa) wa madaraka.
Mukama alitoa kauli mjini Dodoma jana kwenye Ukumbi wa Halmashauri Kuu CCM, wakati akifungua Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM). Hivyo akasema hivi sasa kuna kila sababu za viongozi wa chama hicho kuanzia ngazi zote wapatikane kwa kuchaguliwa na si kupangana kwenye uongozi.
“Unakuta mtu ni Mbunge, M-NEC, mara sijui Mjumbe mtu mmoja anavyeo vitatu hadi vinne, sasa haya mambo ndiyo tunataka kuyarekebisha. Hivyo vijana mnajukumu kubwa la kuhakikisha mnatafuta vijana wenye uwezo mkubwa wa ushawishi kiuongozi ili tujenge chama chetu. Chama chochote makini lazima kijitathmini, kifanye uchambuzi wa kina, ili kiweze kutambua sababu zilizokifanya mambo yake yaende kombo.
Pia kijitambue na kukiri makosa yake kisha ndipo kijisahihishe. Sisi tumefanya hivyo, tumejirekebisha kwa lengo la kuwasema wanyonge, yaani mkulima na mfanyakazi pia kurudisha imani kwa wananchi, maana huwezi kuitenga samaki na maji,” alisema Mukama.
Akizungumzia kauli zinazotolewa na baadhi ya makada wake kuhusu kufanya maamuzi magumu, alisema huwezi kufanya maamuzi magumu bila ya kujitathmini kwanza.
“Maamuzi magumu yanahitaji ufikiri mkubwa. Kila mmoja anakumbuka namna uamuzi wa kuvunja Mkataba wa City Water ulivyotugharimu kugharamia gharama za kutetea uamuzi huo. Uamuzi huo ulitugharimu sh. bilioni 9 kutetea kesi iliyokuwa imefunguliwa na Waingereza na hii yote ni kutokana na ukweli kwamba suala hilo lilifanywa kisiasa, sasa haya ndiyo maamuzi magumu.
Matatizo yetu yanahitaji kufikiri zaidi, hivyo tumieni akili yenu, mjitume bila kukimbia kwenye maamuzi ambayo yanaweza kuwapeleka kwenye matatizo,” alisema Mukama.
Kaimu Mwenyekiti wa UVCCM, Beno Malisa alisema chama hicho kinakabiliwa na tatizo la makundi jambo ambalo linakimaliza chama.
“Chama chetu kimejaa majibizano ya viongozi na jambo hili limeanzia ngazi ya juu, likaja kwetu na nina hofu litakwenda hadi kwa chipukizi wa chama.
Majibizano haya hayana tija kwa chama chetu, kila mtu anataka sifa binafsi, kila mtu anatoka ‘solo’ sasa kila mtu akiamua kutoka ‘solo’ patakuwa hapatoshi hapa. Kimsingi ni kwamba chama chetu sasa maji yamefika shingoni, tukiendelea hivi hivi huko mbele tutakuwa tukiumbuana wenyewe wenyewe, sasa wewe ndiyo Mtendaji Mkuu hivyo unajukumu la kuhakikisha mambo haya yanamalizika,” alisema Malisa.
-Jambo Leo