Mujuni kuzichezesha APR na Tusker

Mwamuzi Israel Mujuni wa Tanzania

Na Mwandishi Wetu

MWAMUZI Israel Mujuni wa Tanzania ameteuliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kuchezesha mechi ya marudiano ya raundi ya mchujo ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya APR ya Rwanda na Tusker ya Kenya itakayochezwa jijini Kigali kati ya Machi 2, 3 na 4 mwaka huu.

Mujuni atasaidiwa na Samuel Mpenzu na Khamis Maswa kutoka Tanzania wakati mwamuzi wa akiba katika mechi hiyo namba 18 atakuwa Louis Hakizimana wa Rwanda. Kamishna wa mchezo huo atakuwa Aboubacar Nkejimana kutoka Burundi.

Nayo Mafunzo ya Zanzibar katika mechi yake ya kwanza katika raundi ya mchujo ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Muculmana de Maputo ya Msumbiji itakayofanyika mjini Zanzibar kati ya Februari 17, 18 na 19 mwaka huu itachezeshwa na waamuzi kutoka Shelisheli.

Bernard Camille ndiye atakayekuwa mwamuzi wa kati huku akisaidiwa na Steve Marie na Gilbert Lista. Mwamuzi wa akiba katika mechi hiyo namba 27 atakuwa Ramadhan Ibada wa Tanzania wakati Kamishna atakuwa Ali Waiswa kutoka Uganda.

Kwa mujibu wa CAF, timu 13 bora zenyewe zimeingia moja katika raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Timu hizo ni Coton Sport (Cameroon), El Ahly (Misri), Djoliba (Mali), Stade Malien (Mali), MAS (Morocco), Raja (Morocco), Sunshine Stars (Nigeria), TP Mazembe (Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- DRC), El Hilal (Sudan), El Merrikh (Sudan), EST (Tunisia), ESS (Tunisia) na Dynamos (Zimbabwe).