Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka amemwaga cheche kuhusiana na ufisadi wa ardhi na kuagiza kama kuna watu wamepora ardhi kwa jeuri ya fedha wajisalimishe mapema.
Prof. Tibaijuka aliyasema hayo jana Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na Waandishi wa habari kuhusiana na shughuli mbalimbali za wizara yake.
“Kama kuna mtu wamepora ardhi kwa jeuri ya fedha, naomba ajisalimishe mapema ili angalau tuweze kuzungumza naye kabla hatujachukua hatua dhidi yake.””Iwapo anataka kuleta jeuri ya fedha sisi hatubabaiki na wala hatutahangaika naye kwani fedha za mboga tunazo,” alisema na kuonegeza “Ni bora wafike ofisini ili tuzungumze, tuwape hata muda kidogo wa kuokoa matofali yao, lakini endapo wataleta jeuri ya fedha tutabomoa kwa kufuata sheria,”
Vile vile aliwataka wananchi wenye taarifa zozote kuhusu uporwaji wa ardhi wazipeleke wizarani ambako zitafanyiwa kazi, na ikibainika ni za kweli sheria itachukua mkondo wake. Akasema wananchi watoe taarifa kwa njia ya mtandao, simu na barua kabla kero haijawa kubwa. Amewataka wananchi kutoa maoni kupitia mijadala kuhusu mahitaji ya nyumba au viwanja.
“Naomba maoni na kero za wananchi zitolewe mapema kabla ya migogoro kukua, tumieni tovuti ya wizara ardhi.go.tz na ya kwangu ni annatibaijuka.org,” alisema Prof. Anna.
“Itabidi tufanye kazi na wananchi, kwani wananchi wasipotusaidia maendeleo shirikishi hatutafika popote,” alisema. “Ninataka kufanya kazi shirikishi kwani wataalamu pekee hawataweza kumaliza matatizo ya ardhi, bado tunahitaji maoni ya wananchi ili kutekeleza majukumu ya ardhi,” alisizitiza.
“Ardhi ni muhimu kuliko fedha, hivi karibuni tulishuhudia uchumi wa Marekani ukiyumba kutokana na kutetereka kwa kampuni mbili kubwa za bima na nyumba,” alisema. Profesa Anna.
Amesema atahakikisha kuanzishwa benki na mikopo ya nyumba, na kuwawezesha wananchi kuipata kupitia mpango wa kurasimisha rasilimali.
Alisema wizara ina mambo mengi yanayopaswa kushughulikiwa na mengine bila kutumia fedha nyingi. Alitoa mfano wa mambo hayo kuwa, namba za nyumba na majina ya mitaa, ambayo yanaonyesha anuani ya makazi ya watu.
Endelea kusoma habari hii katika blogu ya Majira na katika tovuti ya UhuruPublications