NAIBU Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba ametangaza nia yake ya kuwania urais akisema huu ni wakati wa kupisha fikra mpya kuongoza dola, licha ya chama hicho kuzuia kutangaza nia na kupiga kampeni kabla ya muda. January Makamba ni mtoto wa mwanasiasa nguli aliyewahi kushika nafasi mbalimbali za chama tawala na serikalini, Yusuf Makamba.
Makamba, mmoja wa makada wa CCM walioonywa na chama hicho baada ya kutuhumiwa kuanza kampeni mapema, alijipigia debe kuwa iwapo atapitishwa na chama hicho, ataelekeza nguvu kwenye vipaumbele vyake vinne ambavyo ni ajira, huduma za jamii, uchumi imara na utawala bora.
Mbunge huyo wa Bumbuli alisema hayo akiwa Uingereza anakohudhuria mkutano wa sekta ya mawasiliano baada ya kuhojiwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza na baadaye kufafanua nia hiyo katika mahojiano na Mwananchi jana.
“Ni wakati wa fikra mpya kushika dola na mimi ninaona kwamba wazee wakae kando. Mfano awamu moja inapoondoka na wazee walioko katika mfumo wakae kando ili kupisha fikra mpya kuongoza dola,” alisema Makamba ambaye ana umri wa miaka 40.
Mwandishi huyo wa zamani wa hotuba za Rais Jakaya Kikwete, alisema hadi sasa ameshafanya uamuzi kwa asilimia 90 kujitokeza kuwania nafasi hiyo ya juu kuliko zote nchini, bado asilimia 10 katika baadhi ya mambo ambayo anaendelea kuyatafakari, kuzungumza na makundi mbalimbali ya wazee, viongozi wa dini na viongozi waliopita “ili nipate ushauri wao kuhusu namna ya kufanya jambo hili”.
Alipoulizwa iwapo ameshawishiwa au kushinikizwa na watu au ni utashi wake binafsi, Makamba alisema kuwa yote ni mchanganyiko.
“Huwezi kuamka nyumbani na kusema unakwenda kugombea. Kuna msukumo wa wapambe wachache ambao ni lazima ukapime kwa makini kabla ya kuchukua hatua yeyote,” alisema.
“Nchi nzima unakuta inazungumza uwe rais, lazima upime na chagizo hizo ni za kweli au zinatoka wapi. Lakini unaposikia hadi viongozi wa dini, wanafunzi wa vyuo unapokwenda wanakuuliza jambo hilo hilo, unatakiwa utafakari.”
Aliongeza: “Mfano unakwenda Maswa (Shinyanga), Liwale (Lindi), Simanjiro (Kilimanjaro), Wete (Pemba) unaambiwa unafaa, ni muhimu katika hili lakini pia wazee, vijana, viongozi wa dini wanasema unafaa kuwaunganisha Watanzania wote ni jambo la kulitafakari na kulichukulia hatua.”
Februari mwaka huu, Kamati Kuu ya CCM iliwapa onyo kali makada wake sita akiwemo January Makamba ikiwatuhumu kupiga kampeni za urais kwa ajili ya uchaguzi mkuu ujao kabla ya muda.
Makada wengine waliopewa adhabu hiyo ni mawaziri wakuu wa zamani, Frederick Sumaye na Edward Lowasa, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wassira na mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.
Pia makamu mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula aliwahi kukemea tabia ya baadhi ya wana-CCM kutangaza mapema nia ya kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi ujao, akisema ni wasaliti wakubwa ndani ya chama.
CCM pia ilitoa mwongozo na kanuni za uchaguzi ambapo, Ibara 6 (2) (1-5) ya maadili ya viongozi wa CCM inawazuia wanachama kutoa michango, misaada, zawadi za aina yoyote, kukusanya michango na kufanya kampeni bila ya kupata kibali kutoka kamati ya siasa ya halmashauri ya eneo husika.
Kwa mujibu wa kanuni za uongozi na maadili za CCM, toleo la Februari 2010, Ibara 6 (7)(i), ni kinyume kwa wanachama wake kutafuta kuteuliwa kuwania urais kabla ya wakati.
Hata hivyo, Makamba alipoulizwa kwa njia ya simu na gazeti hili alikanusha kuanza kampeni kinyume na onyo walilopewa. “Siyo kwamba ninakiuka onyo tulilopewa na Kamati Kuu. Walichokataza ni kuanza kampeni mapema au kuchukua vijana, wazee, wapambe na waandishi wa habari kupiga kampeni,” alisema Makamba.
Alipoulizwa sababu ya kutangaza nia hiyo ugenini, alijibu: “Hapa ndipo nimeulizwa swali katika mahojiano, hivyo nimeamua kuweka wazi ukweli ulivyo,” alisema Makamba.
Vipaumbele vyake
Makamba alibainisha vipaumbele vyake endapo atateuliwa na CCM kugombea nafasi hiyo kuwa ni pamoja na kushughulikia tatizo la ajira, huduma za jamii, uchumi imara na utawala bora.
Akifafanua vipaumbele hivyo alisema, watu wamekuwa wakizungumzia suala la kutatua tatizo la ajira kwa wembamba na sio kwa mapana, lakini yote haya yanatokana na kipato chao kuwa chini.
“Mazingira katika uchumi bado siyo mazuri, nitahakikisha kila mtu mwenye kipato cha chini anakuwa na kipato cha kati na mwenye kipato cha kati anakuwa na kipato cha juu kwa hali hii vijana wetu hawatakimbilia kuajiriwa, bali watataka kujiajiri wao kwani watakuwa na mitaji kutoka katika vipato vyao,” alisema.
“Kuhusu huduma za jamii kama elimu, afya na maji… na zenyewe yapo mawazo ya kuboresha kwani huwezi kuendesha taifa lisilokuwa na huduma nzuri kwa wananchi.”
Kuhusu suala la uchumi alisema, utaimarika endapo huduma za umeme, usafirishaji na mawasiliano zitaimarika kwani zitawasaidia wananchi kufanya shughuli zao kikamilifu.
“Huwezi kuongoza nchi kama utawala bora haupo. Hapa tutaangalia namna ambavyo tutaendesha Serikali… namna ambavyo haki zinatolewa kwa wananchi kwa wakati,” alisema Makamba.
Aliongeza: “Haya ndio mambo ambayo nimeyawaza na kuona kama changamoto kwangu. Nitakayafanyia kazi kuona Tanzania, kama ni katika ngumi, katika uongozi wangu (Tanzania) iwe inapigana katika uzito wa juu kabisa.”
Pia Makamba amesema mchakato wa Katiba Mpya ulipofikia unahitaji kurudishwa kwa wananchi wakapige kura ya maoni kuamua endapo wanahitaji Muungano na ni muundo wa aina gani wangeupenda.
Awamu ya vijana
Katika mahojiano hayo, Makamba alisema umefika wakati vijana wakashika dola kutokana na mabadiliko yaliyojitokeza katika awamu nne za utawala wa chama chake cha CCM.
Alisema marais wote wanne, Mwalimu Julius Nyerere, Ali Hassan Mwinyi, Benjamini Mkapa na Jakaya Kikwete wamefanya kazi nzuri na kuitambulisha nchi kimataifa, hivyo zinahitajika fikra mpya kuendeleza raslimali nyingi zilizopo.
Kuhusu uzoefu wake
Akizungumzia uzoefu, Makamba alisema hakuna ushahidi wowote kwamba miaka mingi kwenye siasa ndiyo inatengeneza kiongozi mzuri.
“Uongozi mzuri unatengenezwa na haiba, wajihi, dhamira, uwezo, maadili, uhodari, hekima na maarifa. Sifa hizi hazipatikani kutokana na uzoefu wa miaka mingi kwenye siasa hata baadhi ya vijana wanazo,” alisema.
Alitoa mifano mingi duniani ambako vijana ambao hawakuwa na uzoefu kabisa katika nafasi za siasa wameshinda na kubadilisha nchi kama Tony Blair aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza.
“(Rais wa Marekani,) Barack Obama alikuwa seneta kwa miaka mitatu tu, Julius Nyerere alikuwa mwalimu akaingia siasa akaja kupewa uongozi wa nchi akiwa na umri miaka 39 tu,” alisema Makamba. “Kama sasa hivi tuna malalamiko mengi kuhusu jinsi mambo yanavyokwenda, je, tunahitaji kiongozi ambaye kwa miaka 30 amekuwa sehemu ya mfumo tunaoulalamikia? Jibu ni hapana.”
Je, CCM ipo tayari kuwaachia vijana? Akijibu swali hilo, Makamba alisema chama hicho kipo tayari na kimeshatoa fursa kwa vijana kushika nyadhifa za uongozi wa juu, akiwamo yeye.
“Chama chetu (CCM) kinasikiliza umma wa Watanzania na mahitaji yao. Umma wa Watanzania unahitaji mabadiliko makubwa na CCM itaongoza mabadiliko hayo kwa kulipatia Taifa hili uongozi mpya wa kizazi kipya,” alisema Makamba.
Akizungumzia uwezekano wa chama hicho kuamua kutoa fursa hiyo ya juu kwa mwanamke, Makamba alijibu, “Kila mtu anaruhusiwa kugombea.”
Kuendesha kampeni safi
Makamba alisema utakapofika wakati wafuasi wake watafarijika kwa kuwa ataendesha siasa safi wakati wa kampeni.
“Hatutafanya kampeni za maneno bali tutaweka mjadala mkubwa wa masuala mbalimbali yanayolikumba taifa.
“Hatutaeleza mambo juu juu bali tutajikita katika kujenga hoja mfano kama kuondoa tatizo la ajira tutaeleza kwa namna gani, kwa vipi ili watu waone, wapime na kutambua kile unachokieleza na hapa tutakuwa very specific.”
Pia Makamba alisema katika siasa zake hataweka mbele masuala ya kutumia fedha kwani kufanya hivyo kutapunguza weledi katika kutekeleza majukumu kwa wananchi.
“Katika mambo ambayo tunayapinga ni matumizi ya fedha… ni aina ya uongozi ambao hatuutaki bali tunataka kufanya mambo ambayo yataijenga nchi kwa umoja wetu na si matumizi ya fedha,” alisema.
Mchakato wa katiba
Katika mahojiano yake na BBC na baadaye Mwananchi, alisema mchakato wa Katiba ulipofika ni bora ukarejeshwa kwa wananchi.
Alisema hivi sasa kuna pande mbili; upande mmoja unasema serikali tatu nao una hoja na upande mwingine unasema serikali mbili. Wanasiasa wanabishana kwa hoja kwamba kila upande unawakilisha wananchi.
“Kumaliza ubishi wa wanasiasa hatuwezi kuamua kwa sampuli, badala yake tuurudishe kwa wananchi waamue je, wanapenda Muungano uendelee kuwapo na waeleze wangependa wa namna gani.
“Baada ya hapo sasa turudi na kuandika Katiba ambayo nina hakika haitakuwa na ubishi tena kwani ni Watanzania wenyewe ndio watakaokuwa wameamua,” alisema.
Jimboni kwake
Kuhusu jimboni kwake, alisema iwapo hatapitishwa na CCM kuwania urais, atarudi kuendelea kuwatumikia wananchi wa jimbo la Bumbuli kama alivyofanya Rais Jakaya Kikwete mwaka 1995 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), Profesa Mark Mwandosya mwaka 2005.
Mzee Makamba amtakia heri
Akizungumzia nia hiyo, Yusuf Makamba, baba yake Januari, alisema hajasikia kauli hiyo ya mwanae lakini akasema kama ametangaza, anamtakia kila la heri.
“January ni mtu mzima, amesoma… ana nyumba yake…. ana mke… ana uamuzi wake kama ametangaza mimi sijui. Mambo ya Dar es Salaam siyafahamu, lakini kama ametangaza basi sisi tunamtakia kila la heri,” alisema Makamba. “Huku tuliko hata umeme hakuna. Mimi nyumba yangu ninatumia sola na wala watu wa huku hawafuatilii televisheni, sasa hatujui kinachoendelea.
“Karibuni huku mje muone jinsi ninavyovuna maharage, mahindi na ndizi. Hiyo ndiyo kazi ya kufanya. Ukishamaliza kulitumikia taifa, unajikita katika kilimo.”
Chadema, CUF waibua mapya
Akizungumzia uamuzi huo, mkurugenzi wa mawasiliano wa Chadema, John Mnyika alipuuza aliyoyaita majigambo ya Makamba akisema kuwa CCM haina jipya hata ikimsimamisha nani kuwa rais.
“CCM inapaswa kuondolewa madarakani, bila kujali ni nani amesimamishwa kwa kuwa kwa muda mrefu ikiwa madarakani imeelemewa na mzigo wa ufisadi na kansa ya uongozi mbovu katika mfumo wake mzima,” alisema Mnyika na kuongeza:
“Suluhisho ni kuchagua chama mbadala kitakacholeta uongozi bora, sera sahihi, mikakati makini, oganizesheni thabiti kwa maendeleo endelevu ya Tanzania.”
Naye naibu katibu mkuu wa CUF (Bara), Magdalena Sakaya alisema ni ngumu kwa kiongozi makini ndani ya CCM kuleta mabadiliko kwa sababu chama hicho hakina misingi madhubuti ya kutatua matatizo ya Watanzania.
“Nchi hii ni ya demokrasi na inaruhusu mtu kugombea nafasi yoyote. Makamba ametangaza, lakini chama chake ndio kinamwangusha kutokana na kutokuwa makini,” alisema Sakaya.
CHANZO: Mwananchi