Mtoto wa Miaka Minne Abakwa na Kusababishiwa Kifo

PICHA NA MTANDAO

PICHA NA MTANDAO

JESHI la polisi Mkoani Arusha,linawashikilia watu watano kwa tuhuma za kuhusika na tukio la ubakaji wa mtoto mdogo liliotokea juni 20 na kupelekea kifo chake.

Akithibitisha kutokea kwa kifo cha mtoto huyo kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha Charles Mkumbo alisema kuwa tukio hilo lilitokea Juni 20 Majira ya saa tatu usiku ,katika maeneo ya makaburi ya Baniani kata ya Unga Ltd jijini hapa.

Mtoto huyo alifahamika kwa jina la Samira Said mwenye umri wa miaka 4 kabila mnyaturu na mkazi wa Esso, alikutwa amefariki Dunia kandokando ya njia ya watembea kwa miguu karibu na mfereji wa maji machafu umbali wa mita 50 kutoka nyumbani kwao .

“ Siku ya tukio hilo marehemu alikuwa anacheza na wenzake nje kidogo ya nyumbani kwao,na ilipofika majira ya saa 12 jioni kwa mujibu wa marafiki zake (majina yamehifadhiwa)walisema alifika mtu mmoja mwanaume mrefu aliyekuwa amevaa suruali na kumwambia marehemu amfuate akamnunulie pipi,na alipomfuata hakurudi tena.”alieleza Mkumbo.

Kamanda mkumbo anafafanua kuwa ilipofika majira ya saa moja usiku baada ya wazazi wake kuonamtoto wao amechelewa kurudi nyumbani na si kawaida yake kuchelewa walianza kumtafuta kwa kuwataarifu majirani opamoja na kutoa taarifa za mtoto huyo katika msikiti wa Esso, ndipo baadae kidogo wakapokea taarifa za mtoto kuonekana katika njia za watembea kwa miguu katika makaburi ya Baniani akiwa amekufa na walitoa taarifa kituo kikuu cha polisi wilaya ya Arusha mjini.

“Jeshi la polisi lilifika eneo la tukio na kumchukua marehemu huyo na kumfikisha katika ghospitali ya mkoa wa Mount Meru kwa uchunguzi zaidi wa dakatari, na mara baada ya daktari kufanya uchunguzi marehemu alibainika kuwa alibakwa na kuvunjwa shingo kitendo kilichopelekea kifo chake.”alifafanua kamanda mkumbo.

Aliongeza kuwa watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani pindi upelelzi utakapokamilika kwa hatua zaidi za kisheria na tayari marehemu amezikwa Juni 21 katika makaburi ya kwa morombo .

Alitoa onyo kali kwa wanaume wenye tamaa chafu au wanaotumia imani za kishirikina kuacha mara moja tabia hizi chafu za kuwanyanyasa watoto wa kike na kusababisha mauaji kama haya watachukuliwa hatua kali za kisheria.