Mtoto wa Kanali Gaddafi akamatwa

Muttasim Gaddafi

MTOTO wa Muammar Gaddafi aliyekuwa Rais wa Libya aliyeondolewa madarakani kwa nguvu za kijeshi, Muttasim Gaddafi ambaye alifanya kazi kama Mshauri Mkuu wa Usalama wa Kitaifa katika serikali ya babake amekamatwa.

Ofisa mmoja wa Baraza la Mpito la Kitaifa nchini Libya (NTC) amesema Mutassim amekamatwa mjini Sirte na kupelekwa Benghazi japokuwa ofisa mwingine kutoka NTC amesema habari hizo bado hazijathibitishwa.

Hata hivyo raia wa Libya mjini Benghazi na hata Tripoli wamekuwa wakisherekea. Taarifa zinadai kuwa Mutassim alikamtwa akiwa kwenye harakati za kutoroka kutoka mjini Sirte ambao umeshuhudia mapigano makali kati ya wanajeshi wa NTC na wale watiifu kwa Kanali Gaddafi.

Wakuu wa jeshi la NTC wanasema sasa hivi wanadhiti eneo kubwa la mji huo wa Sirte. Ikiwa kweli Mutassim Gaddafi atakuwa amekamatwa, hii itakuwa habri njema kwa baraza la mpito na pigo kwa makundi yaliosalia yanayo mtii kanali Gaddafi.

Inadaiwa kuwa wanajeshi waliokuwa wakipigana na wale wa baraza la NTC mjini Sirte alipozaliwa Kanali Gaddafi wamekuwa wakimlinda Mutassim. Ikiwe ni kweli amekamatwa, Mutassim atakuwa wa mtu wa kwanza wa wa jamaa ya Gaddafi kushikwa.

Mke wa Kanali Gaddafi na watoto wake wakike wapo nchini Algeria na huku kaka yake, Saif al Islam anadaiwa kuwa mafichoni mjini Bani Walid. Raia wengi wa Libya wanaounga mapinduzi haya wanahamu kuona Kanali Gaddafi anakamatwa akiwa hai.