Mtoto Albino Akatwa Mkono Mbeya, Vilio Vyatawala Hospitalini

Mtoto mwenye ulemavu wa ngozi Baraka Cosmas(6) akiwa wodi namba nane Hopaitali ya Rufaa Mbeya ambako amelazwa kutokana na jeraha la kukatwa kiganja cha mkono kwa imani za ushirikina.

Mtoto mwenye ulemavu wa ngozi Baraka Cosmas(6) akiwa wodi namba nane Hopaitali ya Rufaa Mbeya ambako amelazwa kutokana na jeraha la kukatwa kiganja cha mkono kwa imani za ushirikina.

 

=

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro katikati akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Stellah Manyanya kwenye ofisi ya Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa Mbeya Dk. Mpoki Ulisubisya walipotembelea kwa ajili ya kumjulia hali mtoto Albino aliyelazwa baada ya kukatwa kiganja cha mkono wake wa kulia.
Wakuu wa mikoa Stellah Manyanya(Rukwa) Abbas Kandoro(Mbeya) wakiwa katika hospitali ya Rufaa Mbeya kumjulia hali mtoto aliyekatwa kiganja chake cha mkono kwa imani za kishirikina.
NI majira ya mchana saa 7: 30 katika hospitali ya Rufaa Mbeya!! ambako amelazwa mtoto mwenye ulemavu wa ngozi(ALBINO) aliyejeruhiwa kwa kukatwa mkono wake  wa kuume na mtu asiyejulikana huko katika
kijiji cha Kipeta wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa.
Wakuu wa mikoa Abbas Kandoro (Mbeya) na Stellah Manyanya (Rukwa) wakiongozana kumtembelea mtoto mwenye ulemavu wa ngozi Baraka Cosmas (6) ambaye amekatwa kiganja chake cha mkono wa kuume na watu wasiojulikana kisha kuondoka nacho.
Simanzi na majonzi vilitawala katika wodi namba 8 ya Hospitali hiyo yenye sifa ya kuhudumia mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ambapo wagonjwa na wananchi wengine walijikuta wakibubujikwa na machozi walipomshuhudia mtoto huyu asiye na hatia akiwa na mkono usio na kiganja.
Mama wa mtoto huyu Prisca Shaaban (27) ambaye pia alijeruhiwa kwa kupigwa na kitu kwa kupigwa na rungu kichwani anaeleza mkasa uliomsibu siku ya uvamizi.
“Ulikuwa usiku wa manane, mtu aliingia ndani na kunitaka nimpe mtoto aende naye, nilikataa akanipiga na rungu kichwani nikapoteza fahamu, akamkata mtoto kiganja cha mkono wa kulia na kuondoka nacho,’’
Ama kwa hakika ni unyama wa hali ya juu ambao haukustahili kufanyiwa binadamu kwa binadamu mwenzie, katika mazingira ya kawaida ni vigumu kuamini aina hii ya ushirikina kama ina tija kwa wanaofanya ushirikina huu, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Stellah Manyanya ana haya ya kusema;
“Si kweli kama viungo vya Albino ni mali, kwani ingekuwa hivyo hata hao alibino wenyewe wangeanza kuwa matajiri kutokana na hali yao, haya ni mambo ya kishetani ambayo msingi wake sijui unatokana na mazingira gani, serikali itaendelea kupiga vita unyama huu,’’
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mbeya ambaye ni Mwenyekiti wa Wakuu wa mikoa yote nchini alisema kuwa mazingira ya Albino yameendelea kuwa katika hatari kutokana na kukosekana kwa ushirikiano baina ya wananchi kwa kuwa ‘’ wauaji wa albino wapo kati yetu tunaishi na kula nao,’’.
Kiongozi wa wenye ulemavu Claud Mwakyoma alisema kuwa kama serikali ina uwezo wa kuwalinda tembo wasiuawe na majangiri wanashindwaje kuwalindaa binadamu wenzao na kwamba inawezekana ulinzi dhidi ya Albino ni mgumu sana hivyo ni vyema basi wakapelekwa gerezani ili waishi kama wafungwa.
“Naamini tukienda kuishi magereza huko kuna ulinzi wa kutosha kwa kuwa huku nje hatuna ulinzi na tunaendelea kuangamizwa kwa kuchinjwa na kuuawa,’’ alisema Mwakyoma.
Prisca ana jumla ya watoto wanne watatu kati yao ni walemavu wa ngozi ambapo mmoja wao ni huyu aliyekatwa mkono, ameiomba serikali imsaidie kumlinda kutokana na hofu ya maisha aliyonayo.
“Nina watoto wanne Baraka (6) aliyekatwa mkono, Lucia (3) na Shukuru (9) ambapo mtoto pekee ambaye asiye na ulemavu ni Jafar(11),’’ alisema.

Alibainisha kuwa siku ya tukio hilo mumewe Cosmas Lusambo alikuwa ameenda kulala kwa mke mdogo ndipo usiku wa manane alipovamiwa na mtu ambaye alitaka kumnyang’anya mtoto ambaye baadaye alipokataa ndipo alipompiga rungu la kichwani na kumchukua mtoto na kumkata kiganja cha mkono wa kulia.