Mtihani wa mawakala wa wachezaji FIFA Machi 29

Damas Ndumbaro, mmoja wa mawakala wa wachezaji wa FIFA Tanzania

Na Mwandishi Wetu

MTIHANI wa uwakala wa wachezaji (players agent) wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) utafanyika Alhamisi ya Machi 29 mwaka huu saa 10 kamili asubuhi kwenye ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura jijini Dar es Salaam, kutakuwa na jumla ya maswali 20 kwenye mtihani huo, 15 yanatoka FIFA kuhusiana na kanuni za kimataifa za mpira wa miguu na matano yatatoka TFF kuhusiana na kanuni mbalimbali zinazotawala mchezo huo nchini.

Wambura amesema kwa ambao wangependa kufanya mtihani huo utakaokuwa katika lugha ya Kiingereza wanatakiwa kujisajili TFF kwa ada ya dola 50 za Marekani ambapo watapewa utaratibu na maeneo ambapo mtihani huo unalenga. Muda wa kufanya mtihani hautazidi dakika 90.

Hata hivyo ameongeza kuwa mtihani uliopita ulifanyika Septemba 29 mwaka jana ambapo watahiniwa wanane walijitokeza na kufanya mtihano huo. Mpaka sasa Tanzania ina mawakala saba wa wachezaji wanaotambuliwa na FIFA.

“Mawakala hao ni Ally Mleh wa Manyara Sports Management, Damas Ndumbaro, John Ndumbaro, Mehdi Remtulla, Ally Saleh, Yusuf Bakhresa na Said Tully,” alisema Wambura.