Mtanzania Mzalendo Aishauri Serikali Kuhamia Dodoma

Baadhi ya majengo yanaopamba Makao Makuu ya Tanzania, Dodoma.

Baadhi ya majengo yanaopamba Makao Makuu ya Tanzania, Dodoma.

Lorietha Laurence na Rose Masaka (SJMC)

SERIKALI imeshauriwa kuendeleza mchakato wa kuhamisha ofisi zote zake mkoani Dodoma kwenye makao makuu ya nchi yetu ili kuweza kupunguza msongamano wa watu na magari.

Hayo yalisemwa na Mtanzania Mzalendo, John Lyasenga wakati akizungumza na waandishi wa habari leo katika ukumbi wa mikutano Idara ya Habari (MAELEZO) jijini Dar es Salaam.

“Kutokana na jiji la Dar es Salaam kuwa na msongamano wa watu na foleni za magari, kuna umuhimu kwa Serikali kufikiria suala hili la kuhamishia ofisi zake na huduma zingine muhimu kwa mji huo mkuu wa Tanzania kwa ni kwa kufanya hivyo kutaleta fursa kwa wakazi wa mji huo,” alisema Lyasenga.

Aidha aliongeza kuwa faida za kuhamia Dodoma ni pamoja na kuwepo kwa fursa mbalimbali kama vile ajira, kuongeza pato la mkoa kupitia ujenzi wa viwanda vitakavyoongeza uzalishaji na kupunguza maafa kwa jiji la Dar es Salaam kama vile mafuriko kutokana na wingi wa watu.

Mkoa wa Dodoma ina ukubwa wa eneo 41,000 kilomita za mraba na idadi ya watu ni 2,083,588 kutokana na Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012.

Aliongeza kuwa, hali ya hewa ya mkoa huo ni nzuri, ukilinganisha na mkoa wa Dar es salaam wenye kilomita za mraba 1,397 huku hali ya hewa, ikiwa ni joto wastani na idadi ya watu  ikizidi kuongezeka hadi kufikia milioni 4,364,541 sawa na asilimia 4.3 kwa mwaka kutokana na Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012.