n]
MTANDAO wa Wanawake na Katiba Tanzania umewapongeza wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba na hasa wajumbe waliokuwa mstari wa mbele kupigania masuala mbalimbali yaliyokuwa yanapendekezwa na mtandao huo juu ya uwepo wa Katiba inayopendekezwa yenye mtazamo wa kijinsia.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanawake na Katiba Tanzania, Prof. Ruth Meena akizungumza na waandishi wa habari ikiwa ni siku moja baada ya Rasimu ya Katiba inayopendekezwa kuwasilishwa kwenye Bunge Maalum la Katiba Mjini Dodoma tayari kwa zoezi la kuanza kupigiwa kura kifungu kwa kifungu na wajumbe wa bunge hilo.
Prof. Meena alisema Mtandao wa Wanawake na Katiba Tanzania haunabudi kuwapongeza wajumbe wote wa bunge maalum na hasa wale waliowaunga mkono kupaza sauti juu ya madai ambayo waliwasilisha kupitia mtandao wao na njia nyingine mbalimbali kushinikiza katiba inayopendekezwa kuwa na mlengo wa kijinsia ili kutoa usawa wa kijinsia.
Alisema Rasimu ya Katiba inayopendekeza imeonesha mwelekeo wa kutoa usawa wa kijinsia jambo ambalo mtandao huo unaamini ni mafanikio makubwa kwao na kwa jamii inayojali usawa wa kijinsia. Aliongeza kuwa yapo mambo kadhaa ambayo walipendekezwa yatajwe kwenye katiba kama umiliki wa ardhi kumtambua mwanamke na kutajwa kwa umri wa mtoto jambo ambalo wanaamini litapunguza kilio cha ndoa za utoto suala ambalo wanaharakati wa masuala ya kijinsia wamekuwa wakilipigia kelele siku zote.
“…Tunapenda kutoa pongezi kwa wajumbe wote wa Bunge Maalum la Katiba kwa moyo waliouonesha kujali masuala ya kijinsia kwa kiasi chake…tunaunga mkono rasimu ya Katiba inayopendekezwa kwa kuamini ni mwanzo mzuri wa kuonesha usawa wa kijinsia…,” alisema Prof. Meena akizungumza na wanahabari.
Kwa upande wake Mjumbe wa Mtandao wa Wanawake na Katiba Tanzania, Usu Mallya akizungumza alisema licha ya mafanikio yao kwa mtandao wao wamehoji baadhi ya mapendekezo ambayo yamekataliwa na wajumbe hao ilhali yanamuelekeo mzuri juu ya uwajibikaji wa wanasiasa kwa wapigakura wao.
Alisema wameshangazwa na kitendo cha wajumbe wa bunge la katiba kuruhusu kipengele ambacho kimeweka utaratibu kuwa Rais wa nchi anaweza kushtakiwa ilhali wamepinga kipengele za kutoa fursa kwa wapiga kura kumuwajibisha mbunge wao baada ya kumchagua pale wanapoona ameshindwa kuwawakilisha kama walivyokubaliana.