Mtandao wa Wanawake na Katiba Walalamikia Uteuzi Makatibu Wakuu

Mkurugenzi wa TGNP, Lilian Liundi akizungumza kwenye moja ya mikutano ya mtandao huo.

Mkurugenzi wa TGNP, Lilian Liundi akizungumza kwenye moja ya mikutano ya mtandao huo.


SISI Mtandao wa Wanawake wa Katiba na Uchaguzi kwa uratibu wa TGNP Mtandao, tunampongeza Mhe. Dk. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa juhudi zake anazozionesha katika kudhibiti matumizi mabaya ya rasilimali za umma ikiwa ni pamoja na kupunguza ukubwa wa serikali na kusimamia kikamilifu utendaji kazi katika ofisi za umma ili kuongeza ufanisi ikiwamo kuokoa upotevu na ubadhirifu wa pesa za walipa kodi.

Pamoja na kumpongeza Mhe. Rais kwa jitihada za serikali yake za kurejesha utawala bora na serikali yenye safu za viongozi waadilifu, tumeanza kuwa wasiwasi kuhusu dhamira ya kutambua nguvu kubwa za wanawake katika kuwezesha jitihada za awamu hii hasa katika kuleta mabadiliko katika maisha ya Watanzania, wanawake kwa wanaume.

Mtandao wa Wanawake wa Katiba na Uchaguzi tumekuwa tukifuatilia kwa karibu Uchaguzi na Uteuzi wa viongozi katika nafasi mbalimabli za kimaamuzi serikalini. Hii ni pamoja na uteuzi wa Makatibu Wakuu,Mawaziri na Wakuu wa Idara/Taasisi mbalimbali uliofanywa hivi karibuni na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Katika uteuzi huo jumla ya makatibu wakuu na manaibu katibu wakuu walioteuliwa ni 50 idadi
ambayo ni pungufu kidogo ikilinganishwa na mwaka 2014 ambako jumla yao ilikuwa 53; ambapo idadi ya Makatibu Wakuu imeongezeka kutoka 23 mwaka 2014 hadi 29 wakati Manaibu Katibu Wakuu imepungua kutoka 30 mwaka 2014 hadi 21 mwaka huu. Kati ya nafasi zote 50 za walioteuliwa na Mhe. Rais, wanawake ni 10 pekee ambayo ni sawa na asilimia 20.

Tathmini yetu ya jumla ni kuwa, ikilinganishwa na awamu iliyopita, idadi ya Makatibu wakuu na Manaibu Katibu Wakuu wanawake imepungua kwa kiasi kikubwa. Takwimu za mwaka 2014 zinaonesha kuwa, idadi ya wanawake waliokuwa Makatibu wakuu au Manaibu Katibu Wakuu ilikuwa 20 sawa na asilimia 37.7 huku wanaume wakiwa 33 sawa na asilimia 62.3.

Katika uteuzi uliofanyika mwaka huu, jumla ya wanawake Makatibu Wakuu na Manaibu ni 10 sawa na asililimia 20 tu huku asilimia 80 inayobakia ikishikiliwa na wanaume. Kwa kuzingatia takwimu hizo, ni dhahiri kuwa, idadi ya Makatibu Wakuu na Manaibu Katibu Wakuu wanawake imepungua kutoka asilimilia 37.7 mwaka 2014 hadi asilimia 20 mwaka 2015. Hii ni tofauti ya asilimia 17.7 ambayo ni kubwa sana na hivyo kuongeza pengo la jinsia katika nafasi za kufanya maamuzi.

Kwa kuangalia nafasi hizo mbili, utagundua kuwa, kwa upande wa Makatibu Wakuu, kati ya 29 walioteuliwa, wanaume ni 26 sawa na asilimia 89.7% huku wanawake wakipungua kutoka 5 (asilimia 21.7) mwaka 2014 hadi 3 (asilimia 10.3) kwa sasa hivyo wanawake katika nafasi hizo wamepungua kwa asilimia 10. Kwa upande wa Manaibu Katibu Wakuu, idadi ya wanawake imepungua kwa kiasi kikubwa pia. Kati ya Manaibu Katibu Wakuu 21 walioteuliwa wanawake ni 7 tu sawa na asilimia 33.3 ikilinganishwa na asilimia 50 mwaka 2014.

Sisi wanaharakati wa masuala ya jinsia tumeshtushwa na uteuzi huo kwani tulitarajia kuwa kwa kuzingatia usawa wa kijinsia uliofanyika katika nafasi za juu za Serilikali (Rais na Makamu wake) teuzi za nafasi za uongozi zingezingatia usawa wa kijinsia kama suala la msingi hasa katika kuhakikisha kuwa wanawake na makundi mengine wanashiriki kikamilifu katika kufanya maamuzi.

Tanzania kupitia (Tanzania Development Vision 2025) ukurasa wa 16) imetambua kuwa mojawapo ya vichocheo vya ukuaji wa uchumi ni pamoja na jamii yenye muono wa kimaendelea ambapo pamoja na mengine unakuwa na tamaduni wezeshi hususani kwa wanawake na makundi mengine. Sambamba na hilo Mpango wa Miaka mitano wa Maendeleo wa nchi yetu (Tanzania FYDP 2011/12 hadi 2015/16- 2.3.5) unatambua kutokuwepo kwa usawa wa jinsia ni moja ya vikwazo vya maendeleo ya kiuchumi, siasa na kijamii licha ya kwamba wanawake wanaunda zaidi ya asilimia 50 ya idadi yote ya watu nchini. Vile vile MKUKUTA II kupitia kipengele cha 2 imeweka lengo la kuhakikisha haki za binadamu na za makundi maalum kama wanawake, wanaume masikini na watoto zinaendelezwa na zinalindwa. Hii inahusisha haki ya kushiriki katika nafasi mbalimbali za uongozi.

Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020, ambayo serikali iliyoko madarakani inaitekeleza katika aya ya 167 (a), kuhusu wanawake, kimeweka lengo la kuendelea kuweka utaratibu wa kikatiba na kisheria utakaowawezesha wanawake kushika nafasi sawa (50/50) za uongozi katika vyombo vya maamuzi katika ngazi zote. Tunasisitiza kueheshimiwa na kutekelezwa kwa vitendo kwa malengo hayo ili wanawake wapate fursa sawa za kutoa maamuzi juu ya masuala muhimu ya taifa letu. Tunaitaka serikali kutekeleza ahadi zake za kuzingatia usawa wa Kijinsia kama ilivyoainishwa kwenye Ilani ya chama chake.

Tunatoa rai kwa Mhe. Rais na viongozi wote kusimamia kikamilifu utekelezwaji wa mikataba mbalimbali iliyosainiwa na Tanzania hususani ile inayohusu usawa wa kijinsia ili kupunguza pengo lililopo kuelekea usawa wa 50/50 katika nafasi za uongozi. Mikataba hiyo ni pamoja na Mpango Kazi wa Beiging (1995), Mkataba wa Maputo, Mkataba wa Nyongeza wa Jinsia na Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC Gender Protocol) na Tamko la Umoja wa Mataifa la Haki za Binaadamu (1948). Mikataba hii mingi husisitiza mataifa husika kuhakikisha uwepo wa asilimia 50 (au 30 kama kiwango cha chini) kwa wanawake katika nafasi za uongozi na maamuzi.

Ni matarajio yetu kuwa nafasi za uteuzi zilizobaki zitafanyika kwa kuzingatia hayo. Nafasi hizo ni pamoja na uteuzi wa Wabunge (ambao walishaanza kuteuliwa), Mabalozi, Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi na Wakuu wa taasisi na mashirika ya umma kadhalika uteuzi wa wajumbe wa Bodi na Tume mbalimbali katika mashirika na taasisi hizo. Ni muhimu teuzi zote katika mihimili mikuu mitatu ya Bunge, Mahakama na Serikali zizingatie usawa wa jinsia.

Mwisho kama Mtandao wa Mashirika yanayotetea haki za wanawake tutazidi kuendelea kufuatilia, kukumbusha na kushirikiana na serikali ya awamu ya tano katika kuleta maendeleo ya Taifa letu yanayozingatia haki za binadamu na usawa wa jinsia.
Imetolewa na:
Lilian Liundi
Mkurugenzi Mtendaji, TGNP Mtandao
Kny: Mtandao wa Wanawake wa Katiba na Uchaguzi.
Januari 5, 2016