MTANDAO Wanawake na Katiba nchini pamoja na Chama cha Wanahabari Wanawake (TAMWA) wamesema wanaunga mkono Katiba iliyopendekezwa na kujivunia hatua waliopiga katika kudai haki mbalimbali za mwanamke kwenye Katiba hiyo ukilinganisha na ile ya Mwaka 1977.
Mtandao huo umetoa kauli hiyo leo jijini Dar es Salaam katika mkutano na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari kuzungumzia hatua ambayo mtandao huo unaoshirikisha zaidi ya hasasi 50 zinazopigania haki anuai katika jamii.
Akizungumza katika mkutano huo na wahariri wa habari, Mjumbe wa Mtandao huo, Dk. Ave Maria Semakafu alisema harakati za kutetea haki za binadamu na hususani za wanawake na watoto zilipata mwanya katika mchakato wa Katiba uliyomalizika jambo ambalo alisema ni hatua kubwa ya safari ya kumkomboa mwanamke.
Dk. Maria Semakafu alisema kwa kuona mwanya nahatua waliopiga wanaharakati katika masuala hayo, kwa kupitia Mtandao wa Wanawake na Katiba pamoja na TAMWA wanaiunga mkono Katiba Pendekezwa kwa kile kuwa na utofauti mkubwa kimaboresho ukilinganisha na ile ya mwaka 2014. Alibainisha kuwa licha ya mapungufu kidogo yaliopo lakini umoja huo umefanikiwa.
“..Mtandao unatambua kuwa kuna mapungufu yaliopo lakini kubwa zaidi ni kwamba ukilinganisha naKatiba ya Mwaka 1977, Katiba Pendekezwa imemtambua Mwanamke na imempa nafasi stahiki kushiriki katika kujenga, kulinda, kuilinda na kuitetea demokrasia inayozingatia haki za usawa,” alisema Dk. Maria Semakafu.
Akitolea mfano alisema madai ya msingi 12 ambayo mtandao ulipaza sauti kutaka kuingizwa ni pamoja na haki za Wanawake kuainishwa kwenye Katiba Mpya, sheria Kandamizi kubatilishwa, kulindwa kwa utu wa mwanamke, utekelezwaji wa mikataba ya kimataifa kuhusu haki za wanawake na haki sawa katika nafasi za uongozi.
Aliongeza kuwa mambo mengine ni haki za watoto wa kike, haki za kufikia, kutumia, kunufaika na kumiliki rasilimali, haki za uzazi salama, haki za wanawake wenye ulemavu, haki za kufikia na kufaidi huduma za msingi, kuwepo kwa tume ya usawa wa kijinsia na kuwa na mahakama ya familia katika katiba mpya.
“…Kwa kiasi kikubwa katiba iliyopendekezwa imezingatia masuala mengi yaliodaiwa na mtandao. Tunatambua juhudi kubwa zilizofanywa na wanawake na wanaume wote wa Bunge Maalum la Katiba, na kuwapongeza kwa yale yote waliyoyatetea kwa nguvu zote na hatimaye kuzingatiwa katika Katiba,” alisema Dk. Maria Semakafu.
Akizungumza awali kabla ya kumkaribisha Dk. Maria Semakafu, Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA Valerie Msoka alivipongeza vyombo vya habari kwa kukubali kupaza sauti juu ya madai anuai ambayo yalitolewa na wanawake ili kuingizwa kwenye mchakato. “…Tunatambua pia mchango wa vyombo vya habari katika kujenga ufahamu kuhusu mchakato wa katiba na hasa kuhusu kwanini katiba mpya izingatie usawa wa kijinsia.” alisema Msoka.