Wakazi wa wilaya ya Tarime wametakiwa kuachana na vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia hasa mila za ukeketaji na ndoa za utotoni kwa watoto wa kike.
Mwito huo umetolewa hivi karibuni na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akizindua uboreshaji wa Hospitali ya wilaya ya Tarime iliyopo mkoani Mara.
Mama Kikwete alisema ukeketaji unaleta matatizo makubwa ikiwa ni pamoja na kupata matatizo wakati wa kujifungua, mtoto wa kike kupata maumivu makali wakati wa ukeketaji na pia kitendo hicho husababisha kutoka damu nyingi na matokeo yake ni kifo.
“Wazazi na walezi acheni mila hizi ambazo hazina faida kwa wakati huu na ni ukiukwaji wa haki za binadamu bali wasomesheni watoto wenu wa kike ili waweze kuwa walezi bora wa familia zao na jamii kwa ujumla”, alisisitiza.
Aliendelea kusema kuwa katika jamii baadhi ya wanawake wanadhalilishwa, kunyanyasika kijinsia na kupata mateso ya aina mbalimbali kama vile kupigwa, kunyimwa haki ya kumiliki mali na kutokuwa na maamuzi ya matumizi ya mali ya familia hata kama wao ndiyo wazalishaji.
Alisema, “Tabia hizi hazikubaliki kabisa katika Dunia ya leo.Mwanamke anayo haki ya kumiliki mali kwa mujibu wa Katiba ya nchi yetu pia anayo haki ya kufanya maamuzi ya pamoja kwa kile alichozalisha kwani mwanamke ni binadamu na siyo chombo cha kuzalisha mali. Binadamu wote ni sawa”.
Kwa upande wa watumishi wa kada ya afya aliwahimiza kufanya kazi kwa bidii na weledi kwa kuzingatia kwamba miundombinu ya Hospitali hiyo imeboreshwa lengo likiwa ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya hususani akina mama , watoto na wazee.
Mama Kikwete aliwaomba viongozi, kina baba na wadau mbalimbali waliohudhuria uzinduzi huo kushirikiana kwa pamoja ili kupunguza na hatimaye kuokoa kabisa vifo vya akina mama wajawazito na watoto katika wilaya hiyo pia wahakikishe kina mama na watoto wanapata huduma bora za afya.
“Akina mama wajawazito wahudhurie kliniki muda wote wa ujauzio pia hakikisheni wanajifungulia katika vituo vya afya na hospitali. Wapelekeni watoto kliniki hadi watakapotimiza umri wa miaka mitano ili wapate kinga wanazostahili”, aliwasihi.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji wa Tarime Dkt. Calvin Mwasha alisema wazo la uboreshaji wa Hospitali hiyo liliasisiwa na Mkuu wa wilaya hiyo Glorius Luoga alipofanya ziara Hospitalini hapo mwanzoni mwa mwaka huu na kubaini kuna matatizo ya uchakavu mkubwa wa majengo.
Uchakavu wa miundombinu ya maji safi na taka, ubovu wa mfumo wa umeme, uchakavu wa vitanda na matandiko,uchakavu na uhaba wa vifaa tiba na vitendea kazi, uhaba wa madawa, ukosefu wa jengo la utawala na upungufu wa watumishi mbalimbali.
“Wadau mbalimbali wa ndani na nje ya wilaya ya Tarime wakiwemo wafanyabiashara wakubwa na wakati, wachimbaji madini wakubwa (ACACIA North Mara Gold Mine) na wadogo, Taasisi za Umma na binafsi, watumishi wa Umma na wananchi walifanikiwa kuchanga shilingi milioni 345, mashuka 80 na vitanda tisa”, alisema Dkt. Mwasha.
Aliyataja maboresho yaliyofanyika kuwa ni majengo ya wagonjwa wa nje, akina mama na watoto, maabara, upasuaji ambapo mwanzo kulikuwa na chumba kimoja cha upasuaji baada ya maboresho kuna vyumba vinne na jengo la upimaji virusi kwa hiari (VCT).
Wodi za wazazi, magonjwa ya akina mama na upasuaji, akina baba, TB wanaume na wanawake, majengo ya jiko ambalo kwa sasa litatumika kama jengo la kuhudumia wateja wa mifuko ya bima ya afya (CHF na NHIF) na jengo la ufuaji.Ujenzi ambao bado kuanza ni Jengo la utawala na sehemu ya kupumzikia wagonjwa.
Dkt. Mwasha alisema kuna vifaa tiba mbalimbali vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 263 ambavyo vimeagizwa kutoka China kupitia kwa mwenyekiti wa maboresho Peter Zacharia. Kutokana na mahusiano yake mazuri na wafanyabiashara wa huko vifaa hivyo ambavyo bado havijalipiwa vimeshafika wilayani Tarime.
Baadhi ya vifaa hivyo ni mashine ya standard stabilizer moja, oxygen concentrator moja, vitanda 130, baiskeli za kubebea wagonjwa 20, mashine ya kupimia full blood picture moja, BP Machine Digital 50 na nguo za kuvaa wagonjwa.
Hospitali ya wilaya ya Tarime ilijengwa mwaka 1956 tangu kipindi hicho inahudumia wananchi wa wilaya hiyo, Serengeti na Rorya.