RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amewataka mawaziri na maofisa waandamizi wa nchi za Afrika wanaoshiriki katika majadiliano na nchi zilizoendelea kutafuta njia za kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabia nchi kukataa kufarakanishwa ama kugawanywa na nchi tajiri.
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa suala la nchi tajiri kuzisaidia nchi zinazoendelea kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi siyo hisani wala fadhila bali ni wajibu wa nchi hizo tajiri ambazo kimsingi ndio wamesababisha matatizo makubwa ya tabia nchi ambayo dunia inakabiliana nayo.
Rais Kikwete ameyasema hayo leo, Novemba 21, 2013, wakati alipohutubia mawaziri wanaounda Umoja wa Mawaziri wa Afrika kuhusu Mazingira – African Ministerial Conference on Environment (AMCEN) pamoja na Kundi la Maofisa Waandamizi wa Afrika Wanaoshiriki katika Majadiliano kuhusu Mabadiliko ya Tabia Nchi – African Group of Negotiators (AGN) ikiwa ni sehemu ya Mkutano wa Kimataifa wa Mabadiliko ya Tabia Nchi – COP19/CMP9, unaoendelea kwenye Uwanja wa Taifa wa Michezo wa Poland mjini Warsaw.
Rais Kikwete anahudhuria Mkutano huo wa siku tatu, akiwakilisha Bara la Afrika katika nafasi yake ya Uenyekiti wa Kamati ya Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Mazingira (CAHOSCC), nafasi ambayo aliombwa na viongozi wenzake aitumikie mwanzoni mwa mwaka huu. Ataishikilia nafasi hiyo kwa miaka miwili.
Akizungumza na mawaziri hao, Rais Kikwete amesema kuwa ni muhimu kwa Afrika kushiriki katika majadiliano hayo ikiwa na sauti moja, wakikataa kugawanywa ama kufarakanishwa kama namna ya kuwapunguza nguvu katika majadiliano hayo magumu na ambayo bila shaka yanachukua muda mrefu.
“Nimekuja hapa kuwaungeni mkono. Hii ni sawa na vita na nyie ndio askari wa mstari wa mbele. Mimi ni Mkuu wa Majeshi ambaye nimekuja kuwatembeleeni na kuwaunga mkono katika vita hii ngumu ya kuikoa dunia. Kwetu sisi Waafrika, ushahidi wa mabadiliko ya tabia nchi uko wazi kabisa. Leo, tunapata mafuriko hata katika Somalia, tokea lini tukapata mafuriko makubwa ya kiasi hiki jangwani? Huwezi kujua, siku nyingine itakuwa ni Dar es Salaam ama Mombasa.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Ujumbe wangu ni ujumbe wa umoja, kuweni wamoja, msikubali kugawanywa, wala kufarakanishwa kwa njia yoyote ile. Mimi kazi yangu ni kuwatakia mafanikio katika mapambano haya. Tunachokitaka sisi katika Afrika tunakijua, uwezo wa kukitafuta tunao, mnajua tulikotoka na mnajua tunakokwenda. Nawaamini sana, naamini katika uwezo wenu.”
Kuhusu uamuzi wa Mikutano iliyopita wa nchi tajiri na zilizoendelea duniani kuzisaidia nchi masikini zaidi duniani kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi, Rais Kikwete amewaambia mawaziri hao:
“Hili siyo suala la hisani wala fadhila. Huu ni wajibu wao kwa sababu wao ndiyo wameifikisha dunia kwenye vurugu hii ya hatari. Hivyo, ni lazima wabebe wajibu na jukumu la kutusaidia sisi masikini kukabiliana na hali hiyo kwa sababu athari hizo zitamfikia kila mtu na kila nchi hata kama zitaanza kwa sisi tusiokuwa na uwezo mkubwa.”
“Sisi ni kama sungura aliyekutwa amebeba mishale na upinde akiwa njiani kwenda kupambana na tembo. Kila mtu alimcheka. Sisi ni kama sungura anayekwenda kupambana na tembo. Kazi yetu ngumu kweli lakini siku moja, mahali fulani, tembo ataanguka,” alisema Rais Kikwete huku mawaziri hao wakiangua kicheko.
Mara baada ya kumaliza, mazungumzo hayo ya Rais Kikwete yameungwa mkono na mawaziri kutoka nchi za Senegal, Gabon, Uganda, Niger na Angola pamoja na Kamishna wa Maendeleo ya Vijijini na Kilimo wa Umoja wa Afrika (AU) Mama Rhoda Peace Tumusiime.