Na Joachim Mushi
MSANII maarufu wa filamu nchini, Mohamed Mwikongi jina la sanaa ‘Frank’ amejiunga na chama kipya cha siasa cha ACT Wazalendo. Frank amejiunga na chama hicho leo jijini Dar es Salaam akitokea Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Katika hafla hiyo ya utambulisho kiongozi mwingine ambaye ni Mwenyekiti wa kitengo cha vijana Taifa wa NCCR Mageuzi, Deo Meck pia amejiunga na chama cha ACT Wazalendo na kukabidhiwa kadi za chama hicho.
Akiwakabidhi kadi za ACT-Wazalendo, Naibu Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Msafiri Mtemelwa leo Makao Makuu ya ACT alisema wamewapokea wanachama hao wapya kwa mikono miwili na wapo tayari kushirikiana nao ndani ya chama hicho. Alisema kuna idadi kubwa ya vigogo kutoka vyama vingine ambao tayari wameomba kujiunga na chama chao na taratibu zinafanywa kutambulishwa.
“…tendo hili la leo la kuwakaribisha vijana hawa ni mwanzo wa kuwatambulisha wanachama mbalimbali wakiwemo wabunge na viongozi wa vyama waliojiunga nasi baada ya kuvunjwa kwa Bunge. Tayari tunao baadhi ya watu waliokuwa wabunge na wameshajiunga nasi na mchakato wa kuwatambulisha unaendelea katika maeneo mbali mbali nchini,” alisema Mtemelwa.
Akizungumzia mchakato wa uchukuaji fomu kwa ajili ya kugombea nafasi mbalimbali ndani ya chama hicho, Mtemelwa alisema Julai mosi mwaka huu Chama Cha ACT-Wazalendo kilifungua rasmi pazia la uchukuaji fomu za kugombea nafasi mbalimbali zikiweno za Udiwani, Ubunge na Urais.
Alisema tangu kuanza kwa uchukuaji huo wa fomu kumekuwa na mwitikio mkubwa wa wanachama kuchukua fomu na hadi sasa kuna baadhi ya majimbo na kata zina watia azma kuanzia wanne mpaka tisa jambo ambalo alidai ni faraja kwa ACT Wazalendo.
“Kati ya majimbo 265 yakiwamo majimbo mapya 26 yaliyoongezwa hivi karibuni na Tume ya Taifa ya Uchaguzi(NEC), ACT-Wazalendo tumeshakuwa na waweka azma zaidi ya mmoja katika majimbo 226 kwa nchi nzima na tunaamini mpaka kufikia mwisho wa uchukuaji fomu ndani ya Chama majimbo yote 265 yatakuwa yanawatia azma mbalimbali wanaosubiri kupitishwa na chama kwa ajili ya uchaguzi mkuu,” aliongeza Naibu Katibu Mkuu huyo wa ACT Wazalendo.
Alibainisha kuwa kichama mwisho wa kuchukua na kurudisha fomu kwa nafasi ya udiwani ni julai 24, kwa nafasi ya Ubunge mwisho ni Julai 31 na kwa nafasi ya Urais mwisho wa kuchukua na kurudisha fomu ni Agosti Mosi, 2015. “Kwa ngazi ya Taifa Halmashauri kuu itakutana Agosti 13 kwa ajili ya kuteua jina la mgombea Urais wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, pamoja na kupendekeza majina ya wagombea Urais kwenye mkutano mkuu. Agosti 13, Mkutano mkuu utamchagua mtu atakayepeperusha bendera ya Chama cha ACT Wazalendo katika mbio za urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”
“Hivi karibuni tumepokea taarifa kutoka katika miji ya Tarime na Rorya Mkoani Mara kuwa kuna watu wanapita na kutangaza kuwa Chama chetu kimezuiwa kushiriki Uchaguzi kwa muda wa miezi sita.
Tumebaini lengo la upotoshaji huu ni kuwakatisha watanzania tamaa juu ya ukuaji wa Chama Cha ACT-Wazalendo pamoja na dhamira yake nzuri ya kuirudisha nchi katika misingi iliyoachwa na hayati Mwalimu Julius Nyerere.
“Tunawataarifu wananchi kuwa Chama chetu kitashiriki uchaguzi mkuu wa Oktoba 25 mwaka huu kwa kuweka wagombea wa nafasi zote na Chama hakitakuwa tayari kuona sehemu yoyote ya nchi mgombea wa CCM anapita bila kupingwa,” alisisitiza Naibu Katibu Mkuu huyo wa ACT Wazalendo.