MSANII maarufu wa muziki wa kikazi kimpya Dully Sykes juzi aliwaduwaza wapenzi wa muziki wa dansi baada ya kupanda katika jukwaa la Malaika Bend na kuimba wimbo wa bend hiyo pamoja na kupiga kwa ufasaha baadhi ya vifaa vya muziki jambo lililowashangaza wengi na kujikuta akiwainua wapenzi wa muziki vitini na kuanza kumshangilia.
Tukio hilo lilitokea ndani ya ukumbi wa Dar West uliopo Tabata Jijini Dar es Salaam ambapo bend ya Malaika ilikuwa ikifanya onesho lake katika ukumbi huo. Dully alipanda jukwaani baada ya kiongozi wa Malaika Bend Christian Bella alipomkaribisha jukwaani kuwasalimu wapenzi wake ambao wengi walikuwa wakitokea maeneo ya Tabata ambapo ni eneo pia analotoka msanii huyo wa kizazi kimpya.
“…Naomba nimkaribishe Dully apande jukwaani kuwasalimu wanaTabata ambao ni majirani zake, Dully anakaa Tabata tangu siku nyingi sana mi nimeingia Tanzania nimemkuta Dully yupo Tabata hadi leo hii anakaa Tabata,” alisikika Bella akisema mara baada ya Bend yake kupiga nyimbo kadhaa.
Dully alipanda jukwaani na kuanza kuimba moja ya nyimbo za Malaika Bend pamoja na kupigiwa vifaa jambo ambalo liliwanyanyua wapenzi wengi kwenye viti ambao hawakutegemea msanii huyo kumudu miondoko ya bolingo tofauti na miondoko yake. Baada ya kuimba wimbo mmoja aliomba apewe gitaa ambalo pia alilicharaza kisawasawa mithili ya mtaalamu na kushangiliwa.
“…Naomba nimalizie kwa kupiga ‘dram’ ili niwaoneshe wapenzi wangu mimi ninamudu kupiga vifaa mbalimbali,” alisema Dully. Baada ya kuachiwa tena dram alipiga kwa ufasaha hivyo kushangiliwa na wapenzi anuai ndani ya ukumbi huo.
Hata hivyo Dully alikuwa na msanii mwenzake ‘Tunda Man’ ambaye naye alipanda jukwaani na kuwasalimu wapenzi wa miondoko hiyo ya kizazi kipya kwa kuimba mashairi kadhaa ya nyimbo zake.