Na Mwandishi Wetu,
MSANII nyota wa muziki wa bongo fleva, Nasib Abdul a.k.a Diamond Platinum ameingia katika mgogoro na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) baada ya kufanya ‘show’ yake ndani ya Tamasha la Fiesta jijini Dar es Salaam akiwa amevalia sare kama za jeshi hilo pamoja na wacheza ‘show’ wake.
Uamuzi huo wa Diamond kuvaa sare kama za JWTZ unamuingiza moja kwa moja katika mgogoro na Jeshi la Wananchi Tanzania baada ya jeshi kujitokeza na kudai ni kosa kisheria kwa mtu au kikundi chochote kuvaa au kumiliki sare hizo hivyo kufanya hivyo ni kinyume cha sheria.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo jijini Dar es Salaam kutoka Kurugenzi ya Habari na Mahusiano, Makao Makuu ya JWTZ, imeeleza ni kosa kisheria kwa mtu au kundi lolote kuvaa ama kumiliki sare za jeshi hilo na kwa yeyote atakayesubutu kufanya hivyo atapambana na mkono wa sheria.
“…Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) linatoa taarifa kwa wananchi wote kuwa ni kosa kisheria kumiliki au kuvaa sare za JWTZ kwa mtu yeyote asiyehusika. Aidha, kumeonekana matukio kadhaa ya baadhi ya vikundi, ama mtu mmoja mmoja kumiliki au kuvaa sare za JWTZ.
Taarifa hiyo imeendelea kufafanua kuwa kwa yeyote atakayeonekana amevaa ama kumiliki sare hizo sheria itachukua mkondo wake. Taarifa hiyo ya jeshi la Wananchi inamuweka matatani moja kwa moja Msanii Diamond Platinum kwa kitendo chake cha kuvaa na kumiliki sare ambazo zinafanana na zile za JWTZ katika show yake ndani ya Tamasha la Fiesta 2014 lililofanyika jijini Dar es Salaam hivi karibuni.
Hata hivyo taarifa ya JWTZ haikumtaja moja kwa moja msanii Diamond Platinum japokuwa tangazo lililotolewa na jeshi hilo linamgusa na huenda akatakiwa kurejesha sare hizo na kujieleza namna alivyozipata.