Msanii Banza Stone Afariki Dunia Leo Dar..!

Banza Stone

Banza Stone

MSANII maarufu wa muziki wa dansi nchini, Ramadhan Masanja a.k.a Banza Stone amefariki dunia leo mchana jijini Dar es Salaam baada ya kuugua kwa muda mrefu. Msanii Banza ambaye aliwahi kuzushiwa kifo mara kadhaa amefariki leo nyumbani kwao Sinza Vatican jijini Dar es Salaam na ndugu wa msanii hiyo wamethibitisha kutokea kwa kifo chacke.
Nyumbani kwa akina Banza maandalizi ya mazishi baada ya kifo chake

Nyumbani kwa akina Banza maandalizi ya mazishi baada ya kifo chake


Banza stone au mwalimu wa walimu kama alivyopenda kujiita atakumbukwa kwa vibao vyake kama ‘Unapotaka Kuanza Maisha’, Mtaji wa Masikini’, Ujafa Ujasifiwa’, na Mtu Pesa’ na nyingine nyingi alizotunga na kuimba wakati wa uhai wake. Akizungumza mmoja wa kaka wa Banza aliyejitambulisha kwa jina la Ally alisibitisha kifo cha msanii huyo na kudai taratibu za mazishi zinafanywa.

Banza Stone ambaye aliwahi kueleza kwa wanahabari kuwa alikuwa akisumbuliwa na maumivu ya kichwa amewahi kutibiwa katika Hospitali ya Parestina Sinza ya jijini Dar es Salaam na baadaye kupewa mapumziko nyumbani huku akitumia dawa alizopewa na madaktari.

Msanii huyo aliwahi kueleza kwenye vyombo vya habari kuwa ugonjwa unaomsumbua ni fangasi kichwani (ubongo) na shingoni. Habari zinaeleza kuwa tatizo hilo limesababisha msanii huyo kuzidiwa mara kadhaa huku akilalamikia kuumwa na kichwa kupita kiasi hivyo kushindwa kufanya lolote. Aliwahi kuwaomba Watanzania na mashabiki wake kumuombea kwani anaamini katika maombi yao anaweza kurejea katika hali yake.

Miongoni mwa kauli tata ambazo msanii Banza Stone aliwahi kutoa ni pamoja na ile ya kwamba ameota akiwa usingizini kwamba amekaribia kufa, na kwamba kifo chake kitatokana na kuungua ghafla kisha kufariki dunia. Kauli nyingine ni pale aliposema kuwa yeye ni marehemu mtarajiwa na kinachomfanya aendelee kupumua ni kwa sababu ana roho ya paka, kauli aliyoitoa baada ya kuzushiwa kifo na baadhi ya watu akiwa yungali hai. Kauli nyingine ni ile ya kufunga ndoa kimyakimya bila ya watu hasa wasanii wenzake kujua.