Msajili Vyama vya Siasa Kuzitumia Redio za Jamii

Ofisa Mfawidhi Ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa kanda ya ziwa Mwanza, Ludovick Ringia (kulia) akielezea ufanyaji kazi wa sheria mbili za vyama vya siasa kwa wenyeviti wa bodi na mameneja wa redio za jamii nchini wakati wa warsha ya siku tano iliyofadhiliwa na SIDA na kuratibu na UNESCO ambayo imefanyika kwenye kituo cha Redio Sengerema mkoani Mwanza.

Ofisa Mfawidhi Ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa kanda ya ziwa Mwanza, Ludovick Ringia (kulia) akielezea ufanyaji kazi wa sheria mbili za vyama vya siasa kwa wenyeviti wa bodi na mameneja wa redio za jamii nchini wakati wa warsha ya siku tano iliyofadhiliwa na SIDA na kuratibu na UNESCO ambayo imefanyika kwenye kituo cha Redio Sengerema mkoani Mwanza.


Na Mwandishi Wetu, Sengerema

OFISI ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini kupitia Mradi wa kuimarisha Demokrasia na Amani (DEP) itaanza kutoa elimu inayohusu sheria ya vyama vya siasa na sheria ya gharama za uchaguzi kupitia redio za jamii ili kuwawezesha wananchi kutambua wajibu wao katika kulinda amani ya taifa kuelekea katika uchaguzi na wakati wa uchaguzi.

Kauli hiyo imetolewa na Mratibu wa Mradi wa kuimarisha Demokrasia na Amani (DEP) kutoka ofisi ya msajili wa vyama vya siasa nchini, Beatrice Stephano wakati akizungumza na mameneja wa redio hizo katika warsha yao ya siku 5 iliyomalizika mwishoni mwa wiki mjini Sengerema.

Beatrice alikuwa akizungumzia mradi anaousimamia ambao umedhaminiwa na UNDP kupitia UNESCO kwa ajili ya kuelimisha umma wa watanzania kupitia redio za jamii katika kipindi hiki kuelekea uchaguzi 2015.

Alisema uamuzi wa kutumia redio za jamii unatokana na redio hizo kuwafikia wananchi wengi zaidi, hali ambayo wadau katika masuala ya demokrasia wameona kwamba inaweza kutumika kuboresha zaidi uelewa wananchi.

Uelewa huo upo katika sheria za uchaguzi, gharama na kuona wajibu wao wa kumsaidia Msajili wa Vyama vya Siasa kukabiliana na mazingira hatarishi ya amani kabla, wakati na baada ya uchaguzi.

Alisema ni kazi ya Ofisi Msajili wa Vyama vya Siasa kusimamia sheria ya vyama namba tano ya mwaka 1992 ya kusajili vyama na kuviangalia na ile ya namba sita ya mnwaka 2010 ambayo inagusia gharama za uchaguzi.

Mratibu huiyo amesema kwamba timu kutoka Ofisi ya Msajili itafika kwenye redio hizo za jamii na kuzungumza na wananchi kuhusu mambo mbalimbali yanayohusu mustakabali wao katika siasa na kuimariuka kwa demokrasia.

Aidha elimu hiyo inatarajiwa kuwasaidia wananchi kutambua kwamba wana wajibu katika kuhakikisha kwamba menejimenti za uchaguzi zinawajibika pamoja na muuingiliano wake ili kuwa na michakato salama ya cuhaguzi na uchaguzi wenyewe.

Alisema mradi huo wa kuelimisha wananchi ambao unafanyika kwa udhamini wa Unesco  kupitia ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) ni moja ya njia za kufanikisha amani katika kipindi chote kuanzia uchaguzi wa mwisho hadi mwingine.

Alisema wanatumia redio za jamii kwa kuwa redio za kibiashara zimekuwa kikwazo hasa bajeti inapouma kidogo. Alisema mradi huo ambao unafanyika kwa mwaka mmoja ni sehemu ya juhudi za taasisi hiyo za kuliwezesha taifa kuendelea kuwa na utulivu.

Wenyeviti wa bodi na mameneja hao katika warsha hiyo walielemishwa uboreshaji wa masoko na umuhimu wa redio za jamii juu ya matumizi ya Tehama kwa ajili ya kuongeza ufanisi wa kazi na kushirikisha zaidi wananchi.

Aidha Ofisa Miradi ya Mawasiliano, Habari na Tehama wa UNESCO, Al Amin Yusuph akizungumzia mafunzo hayo alisema kwamba mradi huo umekuja wakati muafaka ili kutoa elimu kwa umma, kwani kutokana na tafiti mbalimbali zilizofanywa takribani asilimia 70 ya wananchi wanaoishi vijijini wanasikiliza redio huku asilimia 5 tu ndio wanaangalia runinga.