Msafara wa Dk Bilal wapata ajali Tanga, wawili wafariki dunia

Na Mwandishi Wetu

MSAFARA wa Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk. Mohammed Gharib Bilal umepata ajali na kuua askari wawili waliokuwa katika moja ya gari la msafara huo. Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa mashuhuda wanasema ajali hiyo imetokea eneo la Mombo wilayani Korogwe.

Taarifa zinasema msafara wa Dk. Bilal umepata ajali ukitokea Wilaya ya Lushoto kuelekea Korogwe baada ya kumalizika kwa ziara ya kukagua shughuli za maendeleo alizozifanya Makamu wa Rais wilayani Lushoto.

Gari moja la Jeshi la Polisi Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) likiwa na askari saba kwenye msafara lilishindwa kukata moja ya kona eneo la Mombo na kupinduka. Askari wawili wamefariki dunia huku wengine wakijeruhiwa na wawili kati yao wakiwa katika hali mbaya.

Aidha miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Korogwe, huku majeruhi wakipatiwa huduma na madaktari. Makamu wa Rais alikuwa akimalizia ziara yake mkoani Tanga, ziara aliyoianza Januari 24, 2012 na kuikamilisha Januari 27 wilayani Lushoto.

Wakati huo huo, Dk. Gharib Bilal ametuma salamu za rambirambi kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Inspekta Jenerari Said Mwema na Mkuu wa Mkoa wa Tanga Chiku Galawa, kufuatia ajali ya gari la Polisi lililopata ajali na kusababisha kifo cha askari sambamba na kujeruhi wengine, ajali iliyotokea leo katika barabara itokayo Lushoto kuingia mji mdogo wa Mombo, gari ambalo lilikuwa mwishoni mwa msafara wa Makamu wa Rais uliokuwa ukitokea wilayani Lushoto.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi yake, imesema Makamu wa Rais amesikitishwa sana na tukio hilo na amewapa pole Mkuu wa Jeshi sambamba na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, na anabainisha kuwa tukio hilo limemgusa sana na anawatakia moyo wa ujasiri na uvumilivu kufuatia tukio hili ambalo limekuja katika kipindi ambacho hakikutarajiwa.

“Naamini mkoa wa Tanga na Jeshi la Polisi watatoa huduma zote zinazohitajika kwa wafiwa sambamba na majeruhi, nami binafsi nitafatilia kwa ukaribu,” anasema Makamu wa Rais Dk. Bilal.

Taarifa hiyo imebainisha kuwa Makamu wa Rais anatarajiwa kuondoka mjini Tanga leo kufuatia kuhitajika kusimamia mkutano wa Kamati ya Muungano unaofanyika leo jijini Dar es Salaam.