RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amezindua Mradi Kabambe wa Serikali wa Uwezeshaji Mifugo (Seed Stock) wa kutoa kifuta machozi cha mifugo kwa maelfu ya wananchi katika wilaya tatu za Mkoa wa Arusha mifugo ambao walipoteza mifugo yao wakati wa ukame mkubwa ulioendelea kwa miaka mitatu mfululizo katika wilaya hizo.
Rais Kikwete amezindua Mradi huo katika sherehe kubwa iliyofanyika mjini Longido Februari 19, 2012, ambako amekabidhi ng’ombe jike watano na mbuzi watano kwa kila moja ya kaya 2,852 zilizopoteza mifugo hasa ng’ombe katika wilaya hiyo wakati wa ukame huo mkali ambao ulifikia kilele chake kwa mwaka 2008/2009.
Kiasi cha ng’ombe majike 500 wametolewa kwa wananchi wa Wilaya ya Longido katika sherehe ya leo iliyohudhuriwa na viongozi kutoka wilaya zote tatu wakiwemo viongozi wa Serikali, viongozi wa halmashauri, wabunge, viongozi wa vyama vya siasa na viongozi wa dini.
Katika sherehe hizo zilizohudhuriwa pia na Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk. David Mathayo David na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, William Lukuvi wananchi wa Wilaya ya Longido wamemshukuru kwa dhati, Kikwete na Serikali yake kwa kubuni na kutekeleza Mradi huo wa aina yake ambao haujapata kubuniwa ama kutelekezwa na Serikali yoyote tokea Uhuru.
Chini ya Mradi huo ambao utagharimu kiasi cha sh bilioni 11.2, kaya 6, 127 katika wilaya za Longido, Ngorongoro na Monduli, zote za Mkoa wa Arusha, zitapewa kifuta machozi cha ng’ombe majike watano na dume mmoja (ama mbuzi badala ya dume kama walivyoamua wananchi wa Longido), ili kuwawezesha wananchi kuanza tena kujenga misingi ya mifugo yao ambayo ilipotea katika ukame mkubwa ambao ulifikia kilele chake mwaka 2009.
Mbali na kutoa kifuta machozi cha mifugo, Serikali imekuwa inatoa misaada ya chakula cha dharura kwa wananchi wa maeneo hayo tokea wakati wa ukame huo. Wilaya ya Longido pekee yake mara nane imepokea chakula cha dharura cha kiasi cha tani 11,000 katika kipindi hicho.
Kwa mujibu wa kikosikazi cha Serikali kilichofanya tathmini ya upotevu wa mifugo kutokana na ukame huo, Wilaya ya Longido ilipoteza ng’ombe 231,832, mbuzi 171,435 na kondoo 92,235, Wilaya ya Ngorongoro ilipoteza ngo’mbe 115, 422 na Wilaya ya Monduli ilipoteza ngo’mbe 56,585, mbuzi 39,766 na kondoo 28,883.
Hatua ya utoaji ngo’mbe kwa wananchi wa Wilaya la Longido ambao utafuatiwa na utoaji wa ngo’ombe kwa wananchi wa wilaya za Ngongoro na Monduli, ni utekelezaji wa ahadi aliyoitoa, Rais Kikwete alipotembelea Wilaya ya Longido Agosti 23, mwaka 2009, na kushtushwa na madhara yaliyokuwa yamesababishwa na ukame katika wilaya hiyo. Rais Kikwete alirudia ahadi yake hiyo wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 katika mikutano yake ya kampeni mjini Longido na katika eneo la Namanga.
Kwa mujibu wa Mradi huo, jumla ya ngo’ombe 25, 055 na wastani wa mbuzi 14, 260 (watano kwa kila kaya) watatolewa na Serikali ambako Halmashauri ya Wilaya ya Monduli itapata ngo’mbe 6,184, Halmashauri ya Wilaya ya Longido ng’ombe majike 11, 408 na wastani wa mbuzi 14, 260 wakati Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro itapata ngo’mbe 7, 463.
Akizungumza katika sherehe hizo, Rais Kikwete amesema kuwa ngo’mbe wanaotolewa kwa wananchi siyo fidia ya mifugo yao ambayo ilipotea wakati wa ukame bali ni kifuta machozi tu.
“Hatuna uwezo wa kuwafidia wananchi ngo’mbe wote waliopotea katika ukame ule. Lakini kama Serikali lazima tufanye jitihada za kuwawezesha wananchi wa Masai kurejea katika shughuli yao kuu yaani ufungaji kwa kutoa kifuta machozi tu kidogo. Bila ngo’mbe hakuna Mmasai.”