Na Mwandishi Wetu
SAMPULI tathmini ya matokeo ya mradi wa PREPARE uliokuwa na lengo la kuangalia uwezekano wa vijana kupunguza ngono, imebainisha haja ya elimu ya afya ya uzazi kukabili hali ya sasa ya tabia hatarishi zinazowakabili vijana wadogo.
Matokeo ya awali ya mradi yalionesha kuwa asilimia 10 ya vijana wenye umri wa miaka 12 mpaka 14 ambao ni darasa la tano na sita waliofanyiwa utafiti walikuwa wameshawahi kufanya ngono na asilimia kubwa ikiwa ni kwa kutumia njia ya haja kubwa.
Kauli hiyo imetolewa na mmoja wa watafiti wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi shirikishi cha Muhimbili,Kitengo cha magonjwa na afya ya akili, Lusajo Kajula.
“Vijana wengi walionekana wakifanya ngono ya uke na ya mdomo ikifuatiwa na ngono ya njia ya haja kubwa Kwa wale ambao wameshawahi kufanya ngono, asilimia 6.3 wamefanya ngono ya njia ya haja kubwa wakati asilimia 93.7 hawajawahi.”
Aidha alisema utumiaji wa kondomu ulionekana kuwa mdogo kwa vijana wadogo ambao wameanza kufanya ngono.
“Asilimia 68 ya wale walioanza kufanya ngono hawajawai kutumia kondomu kabisa wakati asilimia 32 wamewahi kutumia kondomu.”
Alisema utafiti huo ni sehemu ya utafiti wa miaka minne ulioshirikisha Vyuo Vikuu vya Makerere cha Uganda, Cape Town na Limpopo vya Afrika Kusini, Bergen na Oslo vya Norway, Maastricht cha Uholanzi na Sussex cha nchini Uingereza.
Mtathmini kiongozi wa mradi huo, Mrema Kilonzo akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Alisema utafiti umeonesha haja ya kutolewa elimu ya afya ya uzazi kwa vijana wadogo ambao bado hawajaanza ngono ili kuchelewesha kuanza ngono kwa mfumo wa kisaikolojia ili waweze kujitambua na kuacha kufuata nadharia za kisayansi pekee ambazo ndizo zinazotumika katika shule mbalimbali kuwaeleza mabadiliko ya miili yao.
Katika utekelezaji wa utafiti huo idadi ya wanafunzi 5,099 walichaguliwa mwanzoni mwa mradi kufanyiwa utafiti huo ambapo wanafunzi 4783 (asilimia 93.9) walifuatiliwa kwa miezi 6 na wengine 4370 (asilimia 85.8) walifuatiliwa kwa miezi 12.
Utafiti ulionesha elimu inayojishughulisha na masuala ya ujinsia na afya ya uzazi kwa vijana wadogo itumie mtazamo mpana utakaoleta mabadiliko ya msingi kwenye misingi ya virekebisho vya mabadiliko ya tabia.
Mradi huo wa PREPARE ulitekelezwa kwenye shule 38 kutoka manispaa ya Kinondoni zilizochaguliwa kwa kutumia taratibu sampuli mtawanyiko zilizopangwa katika makundi mawili ya shule za mwingilio yaani ilikotolewa elimu hiyo zilizokuwa 19 na za kulinganisha zilizokuwa 19.
Ili kuweza kupata matokeo yaliyokusudiwa mradi ulitoa mafunzo kwa walimu watano wakufunzi wa wakufunzi; ulitoa mafunzo kwa walimu watekelezaji 76, na waelimishaji rika wanafunzi 132 na kuelekeza watoa huduma 8 wa afya katika kliniki za huduma rafiki kwa vijana ili kutekeleza muingiliano.
Tathmini iliyotoa majibu ya jinsi utendaji unavyoendelea na ya matokeo ilihusisha shule zote na wanafunzi zaidi ya 6,000 waliowekwa kwenye muingiliano, huku uchambuzi wa tathmini ukihusisha wanafunzi wenye umri wa miaka 12-14, wenye kujua kusoma na kuandika.
Matokeo yaliyotathminiwa ni Mabadiliko katika masuala ya ngono (kuanza ngono) na Kutumia kondomu wakati wa kujamiiana kwa wale waliokwisha anza ngono.
Kwa wastani mradi uliona kwamba mwingilio wa PREPARE ulipunguza uwezekano wa vijana wadogo (wavulana na wasichana) kuanza ngono na kuongeza uwezekanao wa kutumia kondomu kwa wale walioanza.
Hata hivyo, katika utekelezaji wa mradi mabadiliko katika uchukuaji wa hatua yalionekana zaidi miongoni mwa wasichana waliopata mwingilio ukilinganisha na wale ambao hawakupata mwingilio.
Uchukuaji wa hatua ulisababisha tabia ya kutumia kondomu miongoni mwa wanafunzi wa kiume lakini siyo miongoni mwa wanafunzi wa kike.
“Kimsingi tunataka kuwaambia wanahabari kuwa miongoni mwa mafanikio makubwa ya mradi wa PREPARE ni kuchelewesha kuanza ngono miongoni mwa wanafunzi wa kiume na wa kike wenye umri wa miaka 12-14 katika mkoa wa Dar es Salaam, Tanzania;
“Kuongeza uchukuaji wa hatua ulio chanya katika kutumia kondomu kwa jinsia zote na taarifa za ongezeko la utumiaji wa kondomu miongoni mwa vijana wa kiume. “
Mradi huu uliofadhiliwa na Umoja wa Nchi za Ulaya, Programu ya utafiti wa afya umelenga kuangalia mwingilio ulio katika misingi ya utamaduni na jinsia, endelevu, kijamii ili kukuza ujinsia na afya ya uzazi miongoni mwa vijana wenye umri kati ya miaka 12-14 kwa kutumia shule kama njia ya kufundishia.