Mradi wa Football for Hope Kusaidia Watoto na Wasiojiweza

Nembo ya TFF

Nembo ya TFF

MRADI wa Football for Hope kusaidia watoto na wasiojiweza kupitia mpira wa miguu uliofadhiliwa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) mkoani Iringa utafunguliwa rasmi Oktoba 13 mwaka huu. FIFA hutoa mradi huo kwa baadhi ya nchi kwa kuzingatia mambo mbalimbali ikiwemo utawala bora, lakini kwa kupitia taasisi zisizo za kiserikali (NGOs) ambapo kwa Tanzania umepatikana kupitia taasisi ya Iringa Development of Youth, Disabled and Child Care (IDYDCC).

Rais wa TFF, Leodegar Tenga ameishukuru FIFA kwa msaada huo, kwani ni mkubwa na kuongeza kuwa ni matumaini yake utatumika kwa lengo lililopangwa. Amesema mradi huo wa FIFA ambao ni wa kusaidia watoto kielimu na wasiojiweza kwa kupitia mpira wa miguu haukupita moja kwa moja TFF ni mzuri kwani moja ya mambo uliofanikisha ni kuwepo jengo na sehemu ya watoto kucheza.

Ni wastani wa nchi kumi tu duniani kwa mwaka zinapata mradi huo kutoka FIFA, jambo ambalo Rais Tenga amesema linachangiwa pia na uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na shirikisho hilo.

MECHI YA YANGA, MTIBWA YAINGIZA MIL 97/-

Mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) iliyochezwa jana (Oktoba 6 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kati ya Yanga na Mtibwa Sugar imeingiza sh. 97,557,000. Watazamaji waliokata tiketi kushuhudia pambano hilo namba 46 lililochezeshwa na Isihaka Shirikisho kutoka Tanga walikuwa 17,313. Yanga ilishinda mabao 2-0.

Viingilio katika mechi hiyo vilikuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa sh. 23,453,748.95 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 14,881,576.27. Mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja sh. 11,925,635.06, gharama ya kuchapa tiketi ni sh. 3,171,190 wakati gharama za mchezo ni sh. 7,155,381.04.

Kamati ya Ligi sh. 7,155,381.04, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 3,577,690.52 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 2,782,648.18.

*Imeandaliwa na Boniface Wambura Mgoyo, Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)