MRADI mkubwa umezinduliwa Pwani ya Lamu ambao utaziunganisha nchi za Kenya, Ethiopia na Sudani Kusini. Ujenzi wa mradi huo mkubwa wa bandari unatarajiwa kugharimu dola za Marekani bilioni 23 (£14.5bn), na utakuwa Kusini Mashariki mwa pwani ya nchi ya Kenya kwenye Mji wa Lamu mpakani mwa Somalia.
Mradi huo utajumuisha pia ujenzi wa bomba la mafuta, reli na barabara kuunganisha Mji wa Lamu na Sudan Kusini pamoja na Ethiopia. Nchi iliyopata uhuru wake hivi karibuni ya Sudan Kusini ina mipango ya kutumia Lamu kama njia kuu ya kusafirishia mafuta yake.
Rais wa Kenya Mwai Kibaki alizindua mradi huo sambamba na Rais wa Sudan Kusini na Waziri Mkuu waEthiopiaMeles Zenawi. “Sina mashaka kuwa siku hii itakumbukwa katika historia wakati tunapojaribu kuwaunganisha watu wetu na kupata fursa za muhimu za kiuchumi na kijamii kwa ajili ya maishayaoyajayo” Shirika la habari la AFP limemnukuu Rais Kibaki akisema wakati wa sherehe za uzinduzi.
Ikifahamika kama kama Bandari ya Lamu ya usafiri ukanda wa Sudan Kusini Ethiopia (Lapsset), inatarajiwa kumalizika kwa miaka minne ikiwa na gharama za awali kutoka serikali hizo tatu huku mipango ya kuwaalika wawekezaji wa kimataifa ikiwekwa.
Steven Ikuwa, anayesimamia mradi huo aliiambia BBC kuwa mipango hiyo ni mikubwa. “Nina furaha kusema kuwa huu ni mradi mkubwa kabisa ambao tunauanza barani Afrika.”
“Lamu ni urithi ulio hai. Tayari Unesco imetangaza Lamu kuwa Urithi wa Dunia na kuwa eneo lililo katika hatari ya kupotea,” Mualimu Badi kutoka kundi la Save Lamu aliiambia BBC.
“Iwapo watu 500,000 watakuja hapa kama wafanyakazi nadhani tutapoteza hadhi hiyo. ”
Badi pia alisema wenyeji wana wasiwasi wa kukosa makazi kutokana na kutokuwa na uthibitisho kuwa ni wakazi halali wa eneo hilo. Akijibu malalamiko hayo Rais Kibaki ametangaza kuwa wakazi wa eneo hilo watapewa hati za kumiliki ardhi na utawala wake utatoa mafunzo kwa vijana 1,000 kuwaandaa kwa fursa zitakazotokana na bandari hiyo.
-BBC