Na Janeth Mushi, Arusha
MWIMBAJI maarufu wa miondoko ya bongo fleva kwa ‘tune’ na staili ya Kimasai, Abel Rusheraa Motika, almaarufu – Mr Ebbo aliefariki dunia jana saa nne usiku mkoani Arusha anatarajiwa kuzikwa Jumatatu kwa wazazi wake eneo la Masai Camp.
Akizungumza na gazeti hili leo mjini hapa Alois Loshila Motika ambaye ni kaka mkubwa wa Mr. Ebbo amesema marehemu anatarajiwa kuzikwa eneo hilo nyumbani kwa wazazi wake baada ya wanandugu kukubaliana.
“Tumepokea msiba huu kwa majonzi makubwa maana tumepoteza mtu muhimu katika familia na mpenda watu…,” alisema Loshila Motika.
Akizungumzia ugonjwa uliosababisha mauti yake, Alois alisema Mr. Ebbo alikuwa amelazwa siku tatu zilizopita katika Hospitali ya Dreams Seminari ya Kanisa Katoliki, iliyopo Usariver Kata ya Olorien mjini Arusha.
Ameongeza kuwa marehemu ameugua zaidi ya miezi tisa kabla ya mauti yake na amekuwa akitibiwa hospitali mbalimbali ikiwemo Selian KCMC. Amesema ndugu yao alikuwa akisumbuliwa na Kansa ya Damu.
Mr Ebbo msanii ambaye atakumbukwa kwa nyimbo zake kama ‘mi mmasai’, ‘Kamongo’ na nyingine nyingi ameacha mke na watoto watatu wa kike hadi mauti yanamkuta.