Mpambano Mkali wa Ngumi Kufanyika Oktoba 25

Mpambano Mkali wa Ngumi Kufanyika Oktoba 25

Mwandishi Wetu

MPAMBANO mkali wa mchezo wa masumbwi utakaowakutanisha mabondia mbalimbali kutoka kila kona ya Tanzania unatarajia kufanyika Oktoba 25, 2014 katika ukumbi wa Friends Corner Manzese jijini Dar es Salaam. Akizungumzia mpambano huo Mratibu wa pambano hilo ambaye pia ni kocha wa mchezo wa masumbwi nchini, Rajabu Mhamila ‘Super D’ alisema maandalizi yanaendelea vizuri.

Alisema kuwa siku hiyo kutakuwa na mpambano wa mahasimu katika mchezo wa ngumi kati ya bondia Saidi Mbelwa ‘Moto wa Gesi’ na George Dimos pamoja na mpambano utawakutanisha bondia Amani Bariki ‘Manny Chuga’ na Ally Bugingo mpambano unaosubiliwa kwa hamu na wapenzi wengi wa ngumi.

Alisema pambano jingine ni kati ya Juma Fundi atakaezichapa na Hamza Mchanjo wakati Hasani Mandula ataonyeshana kazi na Mohamedi Jaka na Shabani Kaoneka atazipiga na Ibrahimu Maokola anaejiandaa kuwania kucheza ubingwa wa taifa mwishoni mwa mwaka huu Fadhili Boika atazipiga na Godfrey Silver na Habibu Pengo atazidunda na Abdallah Luanje, Kashinde Mohamedi atazidunda na Mohamed Kibaga wakati Sadiki Nuru atakumbana na Mohamed Mbishi.

Akifafanua zaidi alisema katika mpambano huo kutakuwa na ulinzi wa kutosha kabisa kutokana na kujipanga vizuri katika swala hilo kingilio ni shilingi 5000, kwa kila mtu mchezo huu utapambwa na burudani mbalimbali. Siku hiyo pia kutakuwa zikiuzwa DVD mpya za masumbwi ambazo zinaonesha mafunzo mbalimbali ya mchezo wa ngumi yanavyoanza hatua kwa hatua mpaka kujua kitu kamili.