Moto wa Rais Dk Magufuli ‘Wateketeza’ Vigogo Bandarini

Waziri Mkuu wa Tanzania, Majaliwa Kassim akizungumzia agizo la Rais Dk John Pombe Magufuli kwa wanahabari.

Waziri Mkuu wa Tanzania, Majaliwa Kassim akizungumzia agizo la Rais Dk John Pombe Magufuli kwa wanahabari.


Na Raymond Mushumbusi- Maelezo

MOTO wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Joseph Magufuli umeendelea kuwachoma vigogo na sasa umewaangukia vigogo wa bandari, ambapo ametengua uteuzi wa Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi, Dk. Shaban Mwinjaka kuanzia Disemba 7, 2015 na atapangiwa kazi nyingine. Rais Dk. Magufuli pia amevunja Bodi ya Bandari na kutengua uteuzi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Bandari Prof. Joseph Msambichaka na Mkurugenzi Mkuu wa Bandari Bw. Awadhi Massawe.

Aidha amewasimamisha kazi Wakuu wa Vitengo vitano vya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Bandari ya Dar es Salaam kutokana na kashfa ya ukwepaji kodi wa makontena 329 kwenye Bandari ya Dar es Salaam. Uamuzi huo umetangazwa na Waziri Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam.

Wakuu wa vitengo waliosimamishwa kazi katika sakata hilo ni pamoja aliyekuwa Meneja Mapato Bw Shaaban Mngazija ambaye kwa sasa amehamishiwa Makao Makuu Kitengo cha Fedha, Mkuu wa Bandari Kavu (ICD) Bw. Rajab Mdoe, Mkurugenzi wa Fedha Bw.Ibin Masoud na Meneja wa Bandari Msaidizi-Fedha Bw. Apolonia Mosha.

Wengine waliosimamishwa kazi ni Wasimamizi wanane wa Bandari Kavu (ICD) ambao ni Bi. Happygod Naftari, Bw.Juma Zaaar, Bw.Steven Naftari Mtui, Bw.Titi Ligalwike, Bi. Lydia Prosper Kimaro, Bw. Mkango Alli, Bw.John Elisante na Bw.James Kimwomwa ambaye amehamishiwa Mwanza.

Hata hivyo Waziri Mkuu Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa alipofanya ziara ya kushtukiza katika Bandari ya Dar es salaam Novemba 27 mwaka huu aligundua utendaji mbovu ndani ya Bandari ya Dar es salaam na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na katika kufuatilia utekelezaji wa maagizo watendaji wa mamlaka hizo wamesimamishwa kazi kupisha uchunguzi.